Vyama vya Muziki Vyatakiwa Kufuata Taratibu Kabla ya Kukutana na Viongozi wa Serikali
VYAMA vya Muziki nchini vimetakiwa kufuata, Sheria, Taratibu na Kanuni
pindi Wanachama wake wanapopanga kukutana na baadhi ya Viongozi wa
Serikali.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya Lugha, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Bi. Husna Kitogo ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa
Sanaa Wizarani hapo wakati alipokutana na Mashirikisho ya Vyama vya
Muziki nchini.
Bi. Kitogo amesema kwamba kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Wasanii
Wanachama na wasio wanachama kukutana na baadhi ya Viongozi wa juu
wa Serikali pasipo Wizara kupewa taarifa jambo ambalo ni kinyume na
utaratibu na kuwataka kufuata Sheria na utaratibu mzuri wa kufanya
mawasiliano na Wizara kabla ya kufanya hivyo.
“Msifanye kazi kwa mazoea, kwani mnapojiamulia kukutana na Viongozi
wa Serikali pasipo kuijulisha Wizara mnakosea kwani Serikali inafanya kazi
kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, na baadhi ya watu wanaofanya
hivi pindi wanapokwama utaona wanarudi kwetu, jitahidini kujenga
utaratibu hata wakutuletea nakala ya barua ili sisi tuweze kuwasaidia
katika kukutana nao hao viongozi,” alisema Kitogo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Madj wa Muziki
Tanzania (TDMA) Bw. Asanterabbi Mtaki ametaja baadhi ya changamoto
zinazowakabili ni pamoja na Usajili wa Vikundi, vibali vya kufanyia kazi,
masuala ya Haki Miliki (Copy rights), kodi za bidhaa za muziki pamoja na
usimamizi wa mapato ya kazi za sanaa.
Amesema kwamba, baadhi ya Wanamuziki nchini wamekuwa hawatambui
umuhimu wa kujiunga na Mashirikisho pamoja na vyama mbalimbali hali
ambayo inadidimiza tasnia ya sanaa kwani kunapelekea kukosekana kwa
ushirikiano katika kujenga taifa, kutokana na hali hiyo ameishauri Serikali
kuwasimamia wanamuziki ambao bado hawajajiandikisha katika Vyama
kufanya hivyo ili kuleta nguvu ya pamoja katika kupigania haki za Wasanii
nchini.
“Naishauri Serikali kuliangalia suala hili la baadhi ya wasanii
kutojiandikisha katika vyama na ndiyo hawa wasanii ambao wamekuwa
wakikutana kimya kimya na Viongozi wa juu wa Serikali na baadhi ya yao
hawako katika Mashirikisho ama Vyama vya Wasanii, hii ni changamoto
kwetu sisi, tunaiomba Serikali itusaidie kuwapa elimu hawa watu ili wajue
faida na umuhimu wa kujiunga na vyama,” alisema Mtaki.
Naye Mwanamuziki Mkongwe na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki
wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) maarufu kama Bw. Juma Ubao
ameiomba Serikali kuendelea kuzisimamia haki za Wasanii nchini hususani
katika suala zima la Haki Miliki zao kwani ndiyo kilio chao cha muda
mrefu.
“Ushirikiano baina ya Serikali na Vyama vya Wanamuziki nchini uzidi
kudumu na hivyo tunaiomba Serikali itusaidie katika kupunguza kodi kwa
bidhaa za muziki kwani kwa kufanya hivyo kutatuondolea adha ya
kununua vifaa visivyo na ubora, kwani tunajikuta tunanunua vifaa hivyo
kutokana na kushindwa kununua vyenye ubora zaidi vitokavyo nje
kutokana na kodi yake kuwa kubwa.”
Katika kikao hicho, baadhi ya mapendekezo waliyokubaliana ni pamoja na
suala la usajili unaofanywa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)
kutambua uwepo wa Shirikisho la Vyama vya Muziki Tanzania, uboreshaji
wa Sheria pamoja na Sera ya Sanaa, Wasanii kulipwa kutokana na kazi
zao zitumikazo katika baadhi ya Vyombo vya habari nchini pamoja na
Wanafani wote nchini kupitia katika Vyama husika.
Kikao hicho kilichoitishwa na Wizara kiliwakutanisha Wajumbe mbalimbali
toka Chama cha Madj wa Muziki Tanzania (TDMA), Chama cha Muziki wa
Dansi Tanzania (CHAMUDATA), Chama cha Taarab Tanzania (TTA),
Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya (TUMA), Chama cha Muziki wa Injili
Tanzania pamoja na Vyama venginevyo lengo likiwa ni kutambua baadhi
ya changamoto mbalimbali zinazoikabili vyama hivyo.
No comments