TCU yafafanua kuhusu utaratibu mpya wa udahili 17-07-2016
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza utaratibu mpya kwa
watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016/2017 wanaochukua
shahada, huku wanafunzi wengi wakiwa hatarini kukosa nafasi kwa kukosa sifa
na vigezo.
Utaratibu huo mpya umekuja ikiwa ni miezi miwili sasa tangu kutumbuliwa kwa
watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na
kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB).
Sifa hizo ziliwekwa mapema wiki hii katika tovuti ya TCU na kurudiwa jana.
Taarifa hiyo inaonyesha kutolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo,
Eliuta Mwageni.
Kulingana na mtandao wa Mpekuzi, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward
Mkaku, amethibitisha taarifa ya utaratibu huo mpya.
Mkaku alisema utaratibu huo umetolewa baada ya mwaka jana kutumika
mfumo wa wastani wa pointi (GPA) ambao Januari, mwaka huu, Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,
aliagiza ufutwe na kurudishwa ule wa madaraja (division) uliotumika siku zote.
“Mfumo wa udahili uliotumika mwaka jana ulikuwa ni GPA na mwaka huu
utatumika mfumo wa divisheni, ndiyo maana utaratibu huo ukawekwa,” alisema
Mkaku.
Moja ya sifa zinazotakiwa katika udahili wa mwaka huu wa masomo
(2016/2017), ni wahitimu wa kidato cha sita waliomaliza kabla ya mwaka 2014
kuwa na ufaulu wa (D mbili) pointi 4.0.
Mchanganuo ulionyesha kuwa pointi hizo zinatokana na ufaulu wa A = 5; B= 4;
C= 3; D = 2; E = 1.
Taarifa hiyo ilionyesha kuwa ili wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2014
na 2015 wawe na sifa za kudahiliwa, watatakiwa kuwa na alama za ufaulu wa
(C mbili ) pointi 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B+ = 4; B = 3; C= 2; D = 1.
Pia tovuti hiyo ilionyesha kuwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita kwa
mwaka huu, watahitajika kuwa na ufaulu wa alama (D mbili) 4.0 kupitia
mchanganuo wa A = 5; B = 4; C= 3; D= 2; E = 1.
Mbali na sifa hizo, watakaodahiliwa ni wale ambao pia watakuwa na
utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne ambazo ni kuanzia alama nne
za D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+, ikiwa A
=75-100, B+ = 65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39, F= 0-38.
Sifa nyingine zinazotakiwa ni wenye cheti cha NVA daraja la tatu pamoja na
ufaulu wa si chini ya alama nne za D za kidato cha nne au sifa nyingine
zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza la Taifa
la Mitihani (NECTA) au Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Pia watahiniwa hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada
(NTA) daraja la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi (FTC) katika
mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa
wenye stashahada za ualimu, au wastani wa daraja la B+ kwa kitengo cha afya
kama tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na stashahada
nyinginezo.
Sifa nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni kuwa na ufaulu wa daraja la
pili kwa wenye stashahada zisizokuwa za NTA.
Pamoja na hayo, TCU ilisema hakutakuwa na usajili wa mafunzo ya awali
pamoja na yale ya UQF6 yaliyozuiwa kuanzia mwaka wa masomo wa
2016/2017.
Taarifa ya tovuti hiyo iliendelea kusema kuwa maombi yote ya usajili wa
wanafunzi hao wanaotaka kuchukua shahada yanatakiwa kupitia TCU pekee.
“Kwamba tume hiyo imeamua kuwa kuanzia mwaka 2016/2017, maombi yote
ya usajili kwa makundi yote yanayoanzia aya ya 3.0 kwenda juu
wataunganishwa na TCU pekee na walio chini ya hapo hawatahusika na tume
hiyo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia TCU ilisema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa kipengele cha 5(1)(c)(i) cha
katiba ya vyuo vikuu, kifungu cha 346 cha sheria nchini.
“Msingi wa kubadili viwango vya kujiunga na elimu ya juu ni kutokana na
kuwepo maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uwezo wa wahitimu
wanaojiunga na vyuo vikuu mbalimbali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mei, mwaka huu, Profesa Ndalichako aliwasimamisha kazi Katibu Mtendaji wa
TCU, Profesa Yunus Mgaya, kwa kushindwa kuisimamia tume hiyo kutokana na
kuwapo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa, kisha wakadahiliwa katika vyuo
vikuu na kupata mkopo
Wengine aliowasimamisha kazi ni Mkurugenzi wa Ithibati na Udhibiti Ubora, Dk.
Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko na Ofi sa
Msimamizi Mkuu wa Taarifa, Kimboka Stambuli.
Pia Mei mwaka huu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idrisa
Kikula, alitangaza kuwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi
maalumu ya stashahada ya ualimu ambao hawakuwa na sifa.
Alipozungumzia sakata hilo Juni, mwaka huu wakati wa uwekaji wa jiwe la
msingi wa ujenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais
Dk. John Magufuli, aliwaita wanafunzi hao kuwa ni vilaza, na kwamba idadi
kubwa ya waliofukuzwa hawakuwa na sifa stahiki za kudahiliwa kusoma kozi
hiyo.
No comments