Kiwanda cha 21st Century chaungua moto
Kiwanda cha Nguo cha 21st kilichopo Kihonda Morogoro kimewaka moto huku baadhi ya mitambo, nguo na malighafi katika Kiwanda vimeteketea kwa moto.
Akizungumzia moto huo Clement Munisi, meneja uzalishaji wa kiwanda hicho
amesema kuwa, moto huo ulianza saa 12:00 asubuhi leo katika mashine moja
ya kuzalishia nguo.
Amesema, wafanyakazi walijaribu kuuzima kwa kutumia kifaa maalumu cha
kuzima moto (Fire extinguisher ) bila mafanikio.
Munisi amesema kuwa, moto huo uliunguza baadhi ya mitambo na malighafi
zilizokuwa katika chumba kimoja ndani ya kiwanda hicho na kusababisha
hasara kubwa.
Amesema kuwa, moto huo uliendelea kuenea katika vyumba vingine ndani ya
kiwanda hicho jambo ambalo lililosababisha baadhi ya nguo zilizokuwa
zikiendelea kutengenezwa kuungua.
Hata hivyo, hajaeleza thamani halisi ya vitu vilivyoteketea kwa moto.
Ramadhani Pilipili, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Morogoro
amesema kuwa, licha ya kuwahi kufika mapema katika eneo la tukio na juhudi
za kuuzima moto, bado miundombinu ya kiwanda hicho imekuwa kikwazo.
“Miundombinu ya kiwanda ni tatizo kutokana na kukosekana eneo sahihi la
kupitishi mipira ya maji na hivyo kulazimika kutumia muda mwingi kwa kuvunja
ukuta ili kufanikisha zoezi la uzimaji,” amesema.

No comments