Ufafanuzi wa TRA kuhusu ongezeko la thamani kwenye huduma za kifedha

UPOTOSHAJI kuhusu makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika
miamala ya benki na simu za mikononi, uliotangazwa na baadhi ya benki,
umeilazimu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa ufafanuzi na kuzuia
benki hizo kutoza kodi kwa wateja wao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa
TRA, Alphayo Kidata, alihoji kwa nini mabenki yametoa matangazo ya kuanza
kutoza kodi hiyo, wakati hata kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo hazijatolewa.

Kidata alisema pamoja na kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni, lakini muongozo
unaotokana na kanuni bado haujatolewa, ndio maana TRA imeshindwa kuelewa
kwanini taasisi hizo zimetoa taarifa zao kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo ya kutoa matangazo ya kutekeleza sheria hiyo, wakati
kanuni za kutekeleza sheria yenyewe hazijatolewa, Kidata alisema kumeonekana
dalili za nia ovu.

“Tangu lini mmeona benki au taasisi ya fedha inaanza kutoa matangazo ya
utekelezaji wa sheria za serikali? Hii ni kwa sababu ya nia ovu.
“Kuna taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii
kuwa VAT itatozwa kwenye amana ya mwenye fedha kwenye benki. Hii si
kweli,” alisema Kidata.

Usahihi wa kodi

“Juzi Bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 2014
kuanzia Julai mosi mwaka huu kwenye huduma za kifedha kwa kurekebisha
kifungu cha 13 cha jedwali la msamaha wa kodi, lakini taasisi hizo zimekuwa
zikipotosha umma,” alisema.

Alisema kutokana na upotoshaji huo, TRA imeamua kueleza ukweli kuhusu
utekelezaji wa sheria hiyo, ili kuondoa utata na upotoshaji unaohusu utekelezaji
wa sheria hiyo.

Kidata alisema sheria hiyo inalenga kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 18,
kwenye ada ambazo benki zinatoza wateja wake katika huduma mbalimbali
zitolewazo na benki au taasisi za fedha.

“Ukweli ni kuwa kiasi cha VAT kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha
gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha na si kwa
mteja,” alisema.

Akitolea mfano suala hilo, Kidata alisema kama ada ya huduma ya benki
ambayo mteja ametozwa ni Sh 1,000, VAT itakayotozwa kwenye kiasi hicho ni
Sh 152.50 tu na benki kubaki na Sh 847.50 na si kuwaongezea wananchi
mzigo.

“Kiwango hiki cha Sh 152.50 ndicho kitakachorejeshwa serikalini na benki au
taasisi ya fedha baada ya kupunguza VAT iliyolipwa kwenye manunuzi ambayo
yamefanywa kwa benki au taasisi ya fedha husika. Kwa mujibu wa sheria hii,
VAT haitatozwa kwenye riba inayotozwa na benki kwenye mikopo,” alisema.

Alisema kuna maelezo yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji
wa huduma za kifedha, atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala
husika haukupitia kwenye akaunti na kuongeza kuwa taarifa hiyo siyo sahihi,
kwa kuwa ukusanyaji wa VAT husika, utafanywa kwa njia ile ile ambayo
gharama za huduma za kifedha zinakusanywa sasa.

Kidata alisema TRA itatoa maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielektroniki
utakavyofanyika, ili kuwezesha mabenki au taasisi za kifedha kutimiza matakwa
ya kisheria ya VAT ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.

“Hivyo tunazitaka benki na taasisi za fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa
taarifa zisizo sahihi kwa umma, kuacha mara moja vinginevyo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa.

“Kimsingi benki na taasisi za fedha zinazohusika zinaagizwa kurekebisha mara
moja taarifa walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi ya marekebisho
ya sheria hii,” alisema.

Barua BoT

Alisema katika hatua za awali, tayari wamewapa maelekezo Benki Kuu (BoT)
ambayo ni msimamizi wao mkuu, ihakikishe hicho kinachofanyika kinasitishwa
na hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa.

“Mwanzo benki na taasisi hizo za fedha zilikuwa zikichukua tozo yote
wanayotoza, hivyo sasa tumewataka katika hiyo hiyo waliyokuwa wakichukua,
ndiyo watoe kodi na si kumuongezea mwananchi mzigo kwa sababu kila kodi
ina msingi wake na si kila kodi inapopanda, imlenge mwananchi. Sisi tumelenga
hiyo hiyo wanayotoza,” alisema.

Alitoa mwito kwa mtu yeyote mwenye uhakika kuwa ameongezewa makato na
benki au taasisi za fedha kwa madai ya utekelezaji wa sheria hiyo, atoe taarifa
ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.

No comments