Watu Watatu Wanaosadikiwa Kuwa Majambazi Wauawa Katika Jaribio La Uhalifu Wilayani Chunya Mkoani Mbeya
JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA.
Mnamo tarehe 27.04.2016 majira ya saa 20:00 usiku huko katika Kijiji na
Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa
Mbeya, watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliuawa katika
majibizano ya risasi na askari polisi wakiwa katika harakati za kufanya
uhalifu kwenye duka bia la jumla mali ya bwana HAMIS mkazi wa
Matundasi.
Inadaiwa kuwa majambazi hao wapatao watano walikuwa wakitumia
pikipiki mbili huku pikipiki moja ikibeba majambazi watatu na nyingine
majambazi wawili huku wakiwa na silaha aina ya SMG yenye namba
1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine walitaka kufanya uhalifu
kwenye duka la jumla la kuuza bia mali ya HAMISI.
Kutokana na taarifa za siri/intelejensia, Jeshi la Polisi lilijipanga
kukabiliana na majambazi hao na katika majibizano ya risasi, jambazi
mmoja ambaye alikuwa na silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU
1120, risasi 26 kwenye magazine aliuawa baada ya kujeruhiwa kwa
kupigwa risasi tumboni na mguuni na aliweza kufahamika kwa jina moja
BARAKA, anayekadiliwa kuwa na umri kati ya 35 hadi 38, fundi ujenzi
mkazi wa Makongolosi.
Aidha majambazi wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea kijiji
cha Matondo na ndipo askari polisi waliendesha msako mkali kuelekea
kijiji hicho na majambazi hao baada ya kuwaona Polisi waliwasha pikipiki
zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi ovyo ndipo Polisi walijibu
mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi wengine wawili na kukamata
Pikipiki moja yenye namba ya usajili MC 761 AFS aina ya Sanlg
iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao.
Majambazi wengine wawili walikimbia na msako mkali unaendelea ili
kuwakamata. Miili ya marehemu imehifadhi katika Hospitali ya Wilaya
Chunya.
Wito:
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi Butusyo A. Mwambelo anatoa wito kwa wananchi kuendelea
kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri ili kuzuia vitendo
vya kihalifu mapema kabla ya kutokea.
Imesainiwa na:
[BUTUSYO A. MWAMBELO – SSP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
No comments