Fedha za mafunzo kwa vitendo kuchelewa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza
kuwa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo zitatolewa mara baada ya
kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi waliombewa fedha hizo toka
vyuo mbalimbali hapa nchini.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na
waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya ucheleweshwaji wa
fedha hizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Prof. Ndalichako amesema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao
majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya
kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwemo majina ya wanafunzi
waliofariki na waliofukuzwa chuo.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kuna chuo ambacho kilituma ripoti ya wanafunzi
waliofukuzwa chuo mwaka 2013/2014 lakini majina hayo yametumwa tena kwa
ajili ya kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa mwaka huu.
Ameongeza kuwa kutokana na kasoro zilizojitokeza katika majina ya wanafunzi
wanaotakiwa kupewa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo Prof. Ndalichako
amesema kuwa serikali haitatoa fedha mpaka uhakiki wa wanafunzi
wanaotakiwa kupata fedha hizo utakapo kamilika kwa vyuo vyote nchini.
Aidha, Mhe. Ndalichako amesema kuwa majina ya wanafunzi hao hewa
yamewekwa katika mitandao wakitakiwa kujihakiki TCU ili kujiridhisha kama
kweli ni wanafunzi na wanaendelea na masomo.
Hata hivyo , Prof. Ndalichako amevitaka vyuo vikuu kutoa ushirikiano kwa timu
zilizotumwa katika vyuo vyao kufanya uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa
kupata fedha hizo kwani kuna baadhi ya vyuo vimekuwa havitoi ushirikiano kwa
kisingizio cha kuwepo kwenye mitihani.

No comments