Gesi Ya Kupikia Kuagizwa kwa Pamoja Kuanza Septemba

Serikali itaanza kutumia mfumo wa uagizaji wa pamoja wa nishati ya
gesi ya kupikia (LPG), kama inavyofanyika kwa mafuta ya ndege, petroli,
dizeli na mafuta taa ifikapo Septemba mwaka huu.

Akizungumza wakati wa semina ya wadau wa sekta ya mafuta kutoka
mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti
wa Nishati na Maji (Ewura), Godwin Samuel alisema mpango huo
utasaidia kupunguza gharama na bei ya gesi hiyo inayoanza kutumika
kwa kasi majumbani.

Samuel alisema mpango huo pia utaongeza udhibiti wa mapato ya
Serikali katika sekta hiyo inayoshika kasi nchini.

Kuhusu uagizaji wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta ya taa,
Mkurugenzi huyo alisema mchakato unaendelea kuboresha mfumo wa
sasa kwa kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau yatakayotumika
kubadilisha taratibu zilizopo ifikapo Novemba, mwaka huu mikataba ya
sasa itakapomalizika.

“Tunakusudia kuongeza ushindani wenye tija katika uagizaji wa pamoja
wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta taa kwa kuongeza idadi ya
kampuni kulinganisha na kandarasi zilizopo zinazofikia kikomo ifikapo
Novemba mwaka huu,” alisema Samuel.

Kuhusu elimu kwa wadau, Mkurugenzi huyo alisema Ewura inalenga
kuwawezesha kujua na kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika sekta
na biashara ya mafuta ili kuwezesha kila upande kutimiza wajibu
kulingana na sheria, kanuni na taratibu.

“Changamoto zinazoikabili sekta na biashara ya mafuta hayawezi
kutatuliwa na Ewura pekee bali ni kwa ushirikiano wa wadau wote,”
alisema.

No comments