Marufuku watumishi kuwa na tenda serikalini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene amesema
serikali tayari imekataza watumishi wa umma kujiingiza katika kuomba tenda
mbalimbali za serikali na hawaruhusiwi na kama mtu anajihusisha na jambo
hilo basi anakiuka misingi ya sheria.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na East
Africa Radio kuhusu baadhi ya watendaji wa umma ambao wanamiliki kampuni
ambazo zinashiriki kufanya tenda ya serikali na zimekuwa zikifanya vibaya na
kusababisha malumbano baina ya wanachi na halmashauri mbalimbali nchini.

Amesema wamezuia swala hilo kisheria ili kuepuka usumbufu ambao umekuwa
ukijirudia mara kwa mara pindi serikali ifanyapo ukaguzi wa utekelezaji wa
kampuni hizo sambamba na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi
kuhusu utendaji kazi wa kampuni hizo, ambazo zinakuwa zimepewa tenda na
halmashauri mbalimbali nchini.

Amewataka wakurugenzi na viongozi wa mikoa kuzingatia sheria ya manunuzi
inavyoelekeza na tayari wameanza uchunguzi kuwabaini watendaji wasio
waaminifu juu ya swala hilo na pindi watakapogundulika kuhusika na swala hilo
serikali itachukua hatua za kisheria.

Ametoa wito kwa watumishi wote wa serikali kutokujihusisha na swala hilo na
wazingatie katika kusimamia haki na usawa kwa watanzania ambao ndiyo
walipa kodi na watumiaji wa huduma mbalimbali za serikali.





No comments