Askofu Gwajima amjibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemuita muongo


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemjibu katibu
mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemtuhumu kuwa ni mwongo
akisema leseni yake ni ya kuendesha magari makubwa na siyo vibajaji na
maguta.
Akihubiri katika kanisa lake jana, Gwajima bila kutaja jina la Makamba, alisema:
“Siwezi kushughulika na vigari vidogovidogo nyie mnanifahamu, mimi nina
leseni ya kuendesha semi trailer …nadhani mmenielewa,” alisema huku waumini
wake wakimshangilia.
Juzi, Makamba aliwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuwa
Askofu Gwajima ni kiongozi wa dini lakini ni muongo na kuwa uongo wake
unawaudhi hata waumini wake ambao ni wanachama wa chama hicho.
Alisema Gwajima amekuwa akisema uongo kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete
hataki kuachia madaraka ya uenyekiti wa chama hicho, kitu ambacho Rais huyo
mstaafu alikanusha akisema ni yeye alikwenda kumshawishi Dk John Magufuli
kuchukua nafasi hiyo kabla ya muda wa uliopangwa kikatiba.
Katika mahubiri hayo, Gwajima pia alisema mafunzo aliyoyapata tangu akiwa
mdogo ni kuogopa kugombana na watu wa aina tatu, walevi, wazee na
wagonjwa.
“Baba yangu alinifundisha nisigombane na walevi, wazee na wagonjwa kwani
ukimpiga kidogo mtu wa aina hiyo anaweza kufa,” alisema Gwajima.
“Hata nyie waumini wangu nawaomba msigombane na watu wa aina hiyo
kwani mnaweza kupata matatizo,” alisema.
Kiongozi huyo aliongoza mamia ya waumini wake kumuombea Rais Magufuli
kwa kushinda uenyekiti wa CCM akisema kofia hizo mbili zimempa meno ya
kung’ata na zitamwongezea kasi ya kutatua matatizo ya wanyonge nchini.
Rais Magufuli juzi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata
kura zote 2,398 alizopigiwa na wajumbe wa mkutano huo.
Kutokana na ushindi huo, Gwajima alisema Magufuli amepewa meno ya
`kung’ata’ kila upande tofauti na alipokuwa na kofia moja ya urais.
Alisema kwa muda mfupi aliokaa madarakani, elimu ya msingi na sekondari
zimeanza kutolewa bure kitendo ambacho maskini na wanyonge wa nchi hii
wameanza kuuona mwanga.
Alisema ataendelea kumwombea Magufuli kwa sababu kazi anazozifanya
zinawanufaisha wanyonge na maskini ambao kwa muda mrefu walipuuzwa
katika nchi yao.
“Kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti ni zawadi kwetu Watanzania, tuendelee
kumwombea kila siku ili aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi,”
alisema.
Alisema nafasi hiyo mpya itamwezesha kupambana na rushwa tatizo ambalo
ameonyesha kuwa `atalivalia njuga’ hata ndani ya chama hicho.
Mbali na Rais Magufuli, Gwajima aliwaombea pia Makamu wa Rais, Waziri
Mkuu, mawaziri na Spika wa Bunge kwamba Mungu awalinde ili wamsaidie
Rais kutekeleza majukumu yake.
Kwa mwezi mzima, Askofu Gwajima amekuwa akitafutwa na Polisi baada ya
kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais mstaafu Kikwete
afikishwe mahakamani kwa makosa yote yaliyofanyika katika utawala wake.
Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai baadhi ya viongozi wa CCM wametuma
watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Magufuli asipewe uenyekiti ambao
umekuwa ukishikiliwa na Kikwete.
Baada ya sauti hiyo, Gwajima aliondoka nchini kwenda Japan lakini Polisi
waliendelea kumsaka hadi Julai 12 walipomkamata katika Uwanja wa Mwalimu
Julius Nyerere (JNIA), aliporejea. Alihojiwa na kuachiwa siku hiyohiyo




No comments