Walimu 4 wamvua nguo na kumchangia viboko binti wa Kidato cha IV Mbeya huku Mwalimu Mwingine Akimtomasa Sehemu za Siri


VITENDO vya ukatili wa kijinsia na dhuluma dhidi ya watoto wa kike vimekuwa
vikishamiri kila siku pamoja na kuwepo kwa taasisi za kutetea haki za
wanawake na kuanzishwa kwa madawati ya Kijinsia kwenye vituo vya polisi
nchini.

Msichana wa kidato cha Nne mwenye umri wa miaka 17,(jina tunalo)
anayesoma shule moja ya sekondari ya Kata mkoani Mbeya amekumbwa na
kadhia ya kuvuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi
na walimu wanne wa shule hiyo.

Tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo kidogo cha Polisi Mbalizi wilaya ya
Mbeya kwenye jalada la uchunguzi namba MBI/IR/967/2016 na kuwekwa
kwenye taarifa yenye namba MBI/RB/2653/2016 linadaiwa kuwahusisha walimu
wanne akiwemo Mkuu wa shule hiyo pamoja na walimu watatu.

Akizungumza huku akiwa na maumivu makali katika Hospitali Teule ya Ifisi
ambako amelazwa akipatiwa matibabu, mwanafunzi huyo alisema kuwa aliitwa
na mwalimu wa nidhamu aliyemtaja kwa jina la Neema Mwaikenda aliyekuwa
pamoja na Mkuu wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina la Mariamu Mwanisenga na
mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili.

Alisema walimu hao walianza kumuadhibu kwa viboko visivyo na idadi huku
akiwa amechojolewa nguo zake ambapo mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina
la Adili akaanza kumshikashika sehemu zake za siri.

‘’Wakati naadhibiwa na walimu wote, huyu mwalimu wa kiume alianza
kunishika huku chini,na kunitaka niwataje wanaume zangu,nikawa nabana
miguu wakazidi kunishambulia kwa vibao na mateke na fimbo,’’ alisema
mwanafunzi huyo.

Alisema sababu zilizosababisha aadhibiwe ilikuwa ni utoro na kuwa siku moja
alipokuwa shuleni alioneshwa na walimu fimbo na kuelezwa kuwa fimbo hizo
zitamuishia mwilini ndipo akaogopa kufika shuleni kwa siku tatu.
Anafafanua kuwa siku aliyofika shuleni ndipo alipokutana na kadhia ya kupigwa
na walimu wanne hadi alipowaponyoka walimu hao na kukimbilia mitaani na
kujificha.

‘’Niliwaponyoka walimu nikakimbilia kwenye nyumba ya jirani na shule
nikajificha hadi jioni na baadaye kwenda nyumbani, kesho yake mama na dada
walinichukua na kunileta hospitali,’’ alisema.

Mwandishi wa habari hizi alifika shuleni anakosoma mwanafunzi huyo kwa nia
ya kukutana na uongozi wa shuleni hiyo ambapo Makamu Mkuu wa shule hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwansanga alikataa kuelezea chochote.
‘’Mie sijui lolote kwanza mie sio msemaji wa shule, kwahiyo sijui lolote juu ya
taarifa mnazohitaji,’’ alijibu Makamu Mkuu wa shule na kuondoka zake.

Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa Charles Mwakalila alisema kuwa
adhabu aliyopewa mwanafunzi huyo ni kubwa kupitiliza kwa kuwa zipo taratibu
za adhabu kulingana na makosa na kuwa mwanafunzi anapaswa kupigwa
viboko vitatu na viboko visivyozidi sita au adhabu mbadala.
‘’Adhabu aliyopewa ni kubwa, tutafuatilia na waliokiuka taratibu watachukuliwa
hatua za kinidhamu,’ ’alisema Mwakalila.

Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari alipoulizwa
juu ya tukio hili alidai kuwa halijafika ofisini kwake na kuwa kwa sasa yeye
yupo kikazi wilayani Chunya na mara atakapofika ofisini atafuatilia na kuchukua
hatua za kisheria kwa wahusika wa tukio hilo.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Mariamu Mtunguja ambaye alifika
Hospitalini alikolazwa mwanafunzi huyo alisema kuwa amemuangalia
mwanafunzi huyo na kuona namna ambavyo damu imevilia kwenye sehemu
zake za makalio na kwenye mapaja.

Mtunguja alisema kuwa kitendo kilichofanywa na walimu hao ni cha kinyama
ambacho hakipaswi kuvumiliwa na kuwa mara itakapobainika atahakikisha
walimu hao wanachukuliwa hatua za kinidhamu.

Muuguzi Mkuu Msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi Elimati Sanga alisema kuwa
mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Julai 21 saa 7:00 mchana ambapo
alipatiwa matibabu na kulazwa kutokana na majeraha na damu iliyovilia mwilini
sehemu za makalio na mapaja.

‘’Ameshambuliwa sehemu za mapaja, damu na masikio yake hasikii vyema
kutokana na kipigo, anaendelea na matitabu hapa hospitali,’’ alisema Sanga.

Muuguzi Mkuu msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi Elimati Sanga akielezea
madhara aliyopata mwanafunzi anayedaiwa kupigwa na walimu wanne wa
shule ya Sekondari Malama.























"habari hii  Mkwinda Blog."


No comments