Aliyemuua Mwangosi apatikana na hatia.

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemtia hatiani kwa kosa la kuua bila
kukusudia askari wa kikosi cha kuzuia ghasia, Picificus Simon anayetuhumiwa
kumuua mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi huko
Nyororo wilayani Mufindi.

Akisoma mwenendo wa kesi, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk Paul
Kihwelo amesema kuwa mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa kufuatia
ushahidi alioutoa kwa mlinzi wa amani.
Jaji Kihwelo amesema mbele ya mlinzi wa amani mtuhumiwa alikiri kosa hilo
akisema alitenda bila kudhamiria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Maganga ameitaka mahakama hiyo
kumpa adhabu ya kifungo cha maisha wakati Wakili wa Utetezi, Rwezaula
Kaijage aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu ikiwa ni pamoja na
kumuachia huru kutokana na majukumu aliyonayo.
Hukumu ya kesi hiyo itatolewa Julai 27.

No comments