Magufuli aonya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 29 Julai, 2016 ameanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida,
Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambapo amezungumza
na wananchi kwa lengo la kuwashukuru kwa kumpigia kura katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali katika kutatua
kero za wananchi na kuwaletea maendeleo.
Akiwa Mkoani Singida, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth
Magufuli amewasihi watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na
vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya
kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye atathubutu kuchochea
vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.
"Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia
kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama
wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala
sitajaribiwa.
"Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni
wananchi wetu wapate dawa" Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano
tangu aingie madarakani Rais Magufuli ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni
kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu zaidi ya laki moja na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika
bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia
40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
Hatua nyingine ni kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya
waliokuwa wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato
serikalini, kutenga shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya
kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard gauge na pia akazungumzia hatua
zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda
mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi
atakayeendelea kutamba.
Akiwa njiani Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Ikungi na baadaye
amefanya mkutano wa hadhara Singida Mjini ambako amesisitiza kuwa serikali
yake haiko tayari kumvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa Ahadi
na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

No comments