WANAFUNZI CHUO KIKUU KIZIMBANI KWA MAUAJI
WATU watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa vyuo vikuu
vilivyoko jijini Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa
na mashitaka ya mauaji.
Wanafunzi hao ni wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Hussein Mustafa
(26) na wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Haruna Nkuye (24) ambao
wanashitakiwa pamoja na fundi makenika Rajabu Ally (41) wote
wakazi wa Dar es Salaam.
Washitakiwa hao wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo kwenye
tukio la ujambazi katika Benki ya CRDB eneo la Chanika Wilaya
ya Ilala, Dar es Salaam, walisomewa mashitaka na Wakili wa
Serikali Jackson Chidunda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma
Shahidi.
Akisoma hati ya mashitaka, Chidunda alidai Desemba 8, mwaka
jana katika eneo la Chanika, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam,
washitakiwa walimuua Ramadhani Halili, Shan Rajabu na
Thomas Otemu.
Hakimu Shahidi alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu
mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya
kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili
wamuunganishe mshtakiwa Mohamed Ungando ambaye jana
hakuwepo mahakamani.
Awali, mshitakiwa Mustafa aliiomba mahakama imsaidie apate
matibabu kwa kuwa viungo vinamuuma kutokana na adhabu
alizopewa akiwa mahabusu.
Hakimu Shahidi alisema gerezani kuna utaratibu wa matibabu,
kama hatatibiwa kesi itakapotajwa tena aijulishe mahakama. Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu.

No comments