Taarifa: Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA)

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemteua Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara kuwa Makamu Mwenyekiti wa
Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Dkt.
Nyamajeje Calleb Weggoro ambaye muda wake umemalizika.
Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Julai, 2016.

Kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya usafiri wa anga ya mwaka 1977
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo huteuliwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mwenyekiti akitoka
Tanzania Bara, Makamu Mwenyekiti hutoka Tanzania Zanzibar na kinyume
chake.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amempandisha cheo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kedmon
Andrew Mnubi kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).

SACP Kedmon Andrew Mnubi pamoja na makamishna wengine 59 ambao Rais
Magufuli amewapandisha vyeo kuanzia tarehe 16 Julai, 2016 watakula kiapo
cha uadilifu kwa viongozi wa umma kesho jumatatu tarehe 18 Julai, 2016 Ikulu
Jijini Dar es salaam saa tatu asubuhi.

Rais Magufuli atakuwepo wakati Makamishna wote 60 wakila kiapo cha uadilifu
kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo litaendeshwa na Kamishna wa Maadili
Jaji Mstaafu Salome Kaganda.

Wote wakaohudhuria tukio hili wanatakiwa kufika Ikulu kabla ya saa mbili na
nusu asubuhi na wataingia kupitia lango kuu la mashariki (lango la baharini).

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
17 Julai, 2016

No comments