TRA :Mapato Bandarini Yameongezeka

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kupungua kwa mizigo
bandarini kumeathiri si Tanzania pekee bali dunia nzima na kwamba
kubanwa kwa mianya ya wizi kumesababisha kuongezeka kwa mapato
kutoka Sh bil 458 Aprili mwaka huu kufikia Sh bil 517.

Aidha, TRA imesema itaanza uhakiki wa namba za utambulisho wa
mlipakodi (TIN) kutokana na kuwepo watu wenye namba mbili na
wasiohakiki watalazimika kudaiwa kodi na TRA.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana, Kamishna wa TRA,
Alphayo Kidata alisema upungufu huo wa mizigo bandarini umezikumba pia
bandari za Beira, Msumbiji, Mombasa, Kenya na kwingineko na kusababisha
mapato kupungua.

“Lakini sisi pamoja na upungufu wa mizigo bandarini makusanyo yanazidi
kuongezeka kutokana na kuzibwa mianya ya kukwepa kodi, hivyo napenda
kuwapongeza wafanyakazi wote wa mamlaka na kusema kwa sasa hakuna
mtu anayeweza kukwepa kodi na wale waliozoea wakae katika njia kuu,”
alisema Kidata.

Kidata alisema wananchi wanatakiwa kuwaunga mkono kwani sasa kodi
inaonekana katika kufanya shughuli za serikali kama kuboresha
miundombinu pamoja na kutoa elimu bure.

Alisema TRA imefikia na kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa
fedha 2015/16 kwa kukusanya Sh trilioni 13.8 sawa na asilimia 100.04 ya
lengo la kukusanya Sh trilioni 13.4 iliyokuwa imepangwa na serikali.

Kidata alisema katika kipindi cha Juni mwaka huu, TRA imekusanya Sh
trilioni 1.4 sawa na asilimia 107.83 ya lengo la kukuzanya Sh trilioni 1.3
ambapo makusanyo ya mwaka wa fedha 2015/16 ni sawa na ongezeko la
asilimia 23.70 la makusanyo ya mwaka 2014/15.

Akizungumzia mashine za kielektroniki za EFDs, Kidata alisema walipoanza
utoaji mashine hizo zilikuwa 5,703 na mpaka sasa mashine 1,700
zimegawiwa kwa watumiaji na wataanza kupita duka hadi duka kuhakiki
matumizi ya mashine hizo.

Kamishna wa mapato ya ndani, Elijah Mwandumbya, alisema mwaka huu
wa fedha wamejipanga kuhakikisha wanaondoa changamoto kwa mtu
mmoja kuwa na TIN zaidi ya moja hivyo watafanya uhakiki.








No comments