Magufuli achaguliwa kwa kishindo CCM

Mkutano Mkuu wa chama cha Mapinduzi(CCM) umemchagua kuwa Mwenyekiti
wa chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dk John Magufuli kwa kupata kura 2,398 sawa na asilimia 100.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali, pia ulihudhuriwa na wajumbe takribani
asilimia 99 ya wajumbe wote.

Rais Magufuli amewashukuru wajumbe wote wa mkutano huo kwa kumchagua
kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi.
Ameahidi kukisimamia chama cha Mapinduzi kwa weledi kama ilivyokuwa kwa
watangulizi wake.

Dk Magufuli amesema uzoefu wa zaidi ya miaka 40 aliyoupata ndani ya chama
hicho utaweza kumsaidia kuiongoza CCM kufikia malengo yake.
Dk Magufuli ameahidi kukomesha usaliti ndani ya chama hicho akiweka bayana
kuwa wote wanaokisaliti chama hicho hawana nafasi.

Ameahidi kukomesha rushwa ndani ya chama hicho kwani amesema ilifika
kipindi kupata uongozi ndani ya CCM ni lazima uwe na pesa.
Rais Magufuli ameahidi kusimamia rasilimali za chama hicho kwa weledi ili
chama kiweze kujitegemea.

Dk Magufuli amesisitiza azma ya Serikali yake kuhamia Dodoma ambapo
ametoa ahadi kuwa atahakikisha ndani ya kipindi cha utawala wake, Serikali
yote itahamia Dodoma.

Wakati huo huo Rais Magufuli, Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi(CCM)
amesema licha ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahman Kinana
kuwasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake kutokana na mabadiliko ya
uongozi, amemtaka kiongozi huyo kuendelea na wadhifa wake.

Aidha Mwenyekiti huyo wa CCM ameagiza Sekretarieti ya CCM iliyokuwa chini
ya Katibu Mkuu ndugu Kinana, iendelee na kazi yake hadi hapo itakapotolewa
taarifa nyingine.

Mapema kabla ya zoezi la kupiga kura kumchagua Rais Magufuli, Mwenyekiti
mstaafu wa CCM Dkt Jakaya Kikwete alimtaka Mwenyekiti huyo mpya
kushughulikia baadhi ya mapungufu yanayokitia hasara chama ikiwemo kuokoa
mali za chama.

Akitaja baadhi ya mali hizo, Jakaya Kikwete amesema kuna wanachama ambao
wamejimilikisha viwanja vya chama hicho bila utaratibu rasmi na kuwapa
tahadhari ya kuvirejesha katika chama haraka.

Amemtaka mwenyekiti mpya wa chama hicho kushughulikia suala la viwanja
ambavyo bado havijapewa hati ili viendelezwe na kugeuzwa kuwa vitega uchumi
na kuongeza wigo wa mapato ya chama.

Aidha Kikwete aliwakumbusha wakuu wa wilaya kuwa wanapaswa kutambua
mojawapo ya jukumu walilonalo ni kulinda maslahi ya chama katika ngazi ya
wilaya.

“Kuna wakuu wa wilaya wamesema eti wao ni wasomi na kwamba siasa
haiwahusu, lakini wajue kuwa wao ni wajumbe wa kamati za siasa za wilaya,
hivyo wajue kuwa wamewekwa kule kwa makusudi kama kiungo kati ya chama
na serikali”

Aidha, DK Kikwete ameivunia mafanikio aliyoyapata ndani ya uongozi wake wa
kipindi cha miaka 10 ikiwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka
wanachama 5,433,425 mwaka 2006 hadi kufikia wanachama 8,782,833 mwaka
huu.

Amesema kiwango hicho cha wanachama ni mtaji mkubwa katika uchaguzi, kwa
kuwa chama kinakuwa kinaingia katika uchaguzi kikiwa na kura zaidi ya milioni 8

Jambo lingine ni kufanikisha kujenga ukumbi mkubwa na wa kisasa wa chama
hicho ulioko Dodoma kwa ajili ya mikutano, na kumtaka mwenyekiti ajaye
aendelea kumalizia ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya chama hicho.

Mafanikio mengine aliyoyataja Kikwete ni kuhakikisha chama hicho kinaendelea
kushinda katika chaguzi mbalimbali ikiwemo zile za serikali za Mitaa ambapo
mwaka 2009 chama hicho kilishinda kwa zaidi ya asilimia 90 na mwaka 2014
kikishinda kwa asilimia 80.

Mbali na mafanikio hayo, Kikwete ametaja baadhi ya changamoto alizokutana
nazo ikiwa ni pamoja vikwazo viwili vikubwa kutoka kwa wananchama.
Vikwazo hivyo ni pamoja na wanachama kutohudhuria vikao na la pili
wanachama kutolipa ada.

Amesema wanachama wengi hawalipi ada zao na wengine wanasubiri hadi
wakati wa kampeni ili walipiwe na wagombea, huku akieleza kuwa endapo
wanachama wangekuwa wanalipa ada zao kwa uaminifu, basi chama hicho
kingeweza kukusanya hadi bilioni 10.5 na kuacha kuendesha chama kwa
kutegemea ruzuku ya serikali.

Amesema wakati mwingine chama kinategemea michango ya wafanyabiashara
ambao nao huchangia chama wakati wa kampeni pekee.
“Wakati wa uchaguzi wafanyabishara wanatuchangia sana, wanasema
wanataka CCM iendelee kubaki madarakani, lakini uchaguzi ukiisha hatuwaoni,
hata simu zetu hawapokei” Amesema Kikwete.

Kikwete pia ametumia fursa hiyo kuelezea sababu kubwa ya chama hicho
kulegalega kuwa ni kutokana na viongozi wa ngazi mbalimbali kutowafikia
wanachama wao kama ambavyo wapinzani wamekuwa wakifanya, na
kumshauri mwenyekiti mpya kuongeza msukumo ili viongozi wawe wanatoka
katika kueneza kazi nzuri zinazofanywa na chama hicho.

Mbali na hayo Kikwete ameendelea kukiri kuwa nusura chama kivujike mwaka
2015 kutokana na hali ya kisiasa ilivyokuwa lakini amefanikiwa kukivusha
salama.

“Katika historia ya CCM hakuna wakati ambao chama kilipata tishio la
kuanguka kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini haikuwa hivyo, na badala yake
kimekuwa imara zaidi”

Amekanusha taarifa kuwa alikuwa anakataa kuachia nafasi hiyo na kusema
kuwa si kweli, bali Rais Magufuli ndiye aliyekuwa anakataa kupokea kazi hiyo,
na yeye kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi akiwemo Makamu Mwenyekiti
Bara Philip Mangula walifanya kazi ya kushawishi hadi Magufuli akakubali.

Amewashukuru wanachama wa chama hicho kwa kumpa ushirikiano kwa kipindi
chote cha miaka 10 na kutaka wanachama hao kuendelea kumpa ushirikiano
zaidi mwenyekiti mpya Dkt John Magufuli.

John Cheyo Mwenyekiti wa UDP na Augustino Mrema Mwenyekiti wa TLP ni
miongoni mwa viongozi wa vyama 12 waliohudhuria mkutano huo.
Aidha viongozi mbalimbali wa kisiasa wamepongeza uchaguzi huo wa CCM
uliomalizika kwa amani.

Mmoja wa viongozi hao ni Zitto Kabwe kiongozi wa ACT Wazalendo ambaye
amempongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa
Mwenyekiti wa CCM.

Zitto amesema uchaguzi huo wa CCM unapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa
vyama vyote vya siasa kuwa na utaratibu wa kuachia madaraka kila baada ya
miaka kadhaa.

Aidha amemtaka Rais Magufuli, Mwenyekiti mpya wa CCM kulegeza msimamo
wa kuzuia mikutano ya vyama vya siasa kwani bila mikutano hiyo vyama vya
siasa kikiwemo chama chake, vitaathirika

No comments