Mtoto aliyewekewa ‘mashine’ kwenye moyo aanza mazoezi
Mtoto Happiness John Mkazi wa Seliani Arusha aliyefanyiwa upasuaji kwenye
moyo na kupandikiziwa kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo
(pacemaker), ameanza mazoezi.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Sulender Kuboja aliyeshiriki
upasuaji huyo alisema jana kuwa hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na
wameanza kumfanyia mazoezi mepesi.
Dk Kuboja alisema kwa kawaida mgonjwa yeyote aliyefanyiwa upasuaji
anapaswa kufanyiwa mazoezi mepesi na kwamba kwa mtoto, mazoezi
anayofanyiwa ni ya kukaa, kusimama na kutembea kidogo.
“Hali yake inaonekana kuendelea vizuri sana... nimetoka kumfanyia vipimo
muda mfupi uliopita kifaa kile kinafanya kazi vizuri na maendeleo yake
yanaridhisha sana,” alisema Dk Kuboja.
Alisema mtoto huyo anaweza kuongea na hata kula chaku- la, hali aliyosema
inaonyesha nafuu nzuri kwake.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Elitruda Malley alisema anaridhishwa na
maendeleo ya afya ya mwanaye kwa kuwa tangu afanyiwe upasuaji huo juzi,
hali yake imeonekana kuimarika kwa haraka.
Mama huyo alisema tangu awekewe kifaa hicho, mwanaye amekuwa
mchangamfu, hali aliyosema inamtia moyo na kumpa matumaini makubwa.
“Ingawa yupo kwenye oxygen, lakini namshukuru Mungu kwani anaonekana
anapata nafuu nzuri, anatabasamu na kuongea vizuri kabisa na ana furaha
sana, shauku yake ni apone ili aende shule kama watoto wengine,” alisema
Malley.
Aliongeza kuwa mtoto huyo amekuwa akila vizuri na kumpa moyo kwani mwili
wake unaonekana kuwa na nguvu na afya nzuri.
“Madaktari wapo karibu wakifuatilia afya ya mtoto kwa ukaribu, wanampa
chakula, wanamfanyia mazoezi ya kukaa na kushuka chini, anaonekana kuwa
na nguvu na mwenye maendeleo mazuri. "
Alisema jambo linalompa faraja ni kuona jinsi madaktari wote wanaomuhudumia
mtoto huyo wanavyofanya kazi hiyo kwa upendo na bidii.
Juzi, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) ilifanikiwa kumpandikiza mtoto huyo mwenye umri wa
miaka mitano kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker)
kinachoendeshwa kwa betri.
Hayo ni mafanikio ya pili kwa taasisi hiyo ya kisasa ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati baada ya Mei 24 na 25, mwaka huu kufanikisha operesheni kwa
wagonjwa 18 bila kuusimamisha moyo

No comments