Kilio cha Mrema Chasikika Ikulu, Rais Dk Magufulia Ampa Kazi
KILIO cha muda mrefu cha Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania
Labour Party (TLP), Agustino Lyatonga Mrema kuomba asisahaulike katika
ufalme wa Rais Dk John Pombe Magufuli kimesikika na hatimaye
amekumbukwa na rais kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa
ya Parole nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu
Lyatonga ameteuliwa rasmi na Rais Magufuli kushikilia nafasi hiyo kwa
kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 16, 2016.
Kilio cha Mrema kilianza kusikika baada ya kuona mambo yanakwenda
kombo kwa upinzani mkubwa katika nafasi ya ubunge aliogombea, dhidi ya
Mbunge wa sasa wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia aliyemshinda katika
uchaguzi mkuu uliopita.
Akiwa kwenye kampeni Jimbo la Vunjo Mrema licha ya kuwa na mgombea
urais katika chama chake, alimnadi Rais Dk. Magufuli alipopita katika
jimbo hilo jambo ambalo lilivuta hisia za wengi, huku akimuomba
amkumbuke katika ufalme wake (uongozi).
Hata hivyo Mrema alizungumza kwa masihara huku akimuacha Dk
Magufuli akicheka kwa furaha kutokana na kauli hiyo ya Mrema. Mrema
alifanya tukio hilo kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu baada ya
kusimamisha msafara wa kampeni wa mgombea huyo wa CCM ulipopita
katika Jimbo la Vunjo.
Wengine walioteuliwa katika uteuzi wa Rais Dk. Magufuli ni pamoja na
Profesa William R. Mahalu ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Prof.
Angelo Mtitu Mapunda anayekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu.
Rais Dk Magufuli pia amemteuwa Bi. Sengiro Mulebya kuwa Kamishna wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Oliva Joseph Mhaiki kuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Winifrida
Gaspar Rutaindurwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC),
Dk. Charles Rukiko Majinge kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Hospitali ya Taifa Muhimbili na Dk. Julius David Mwaiselage kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
Wakati huo huo, Rais Magufuli pia amewapandisha vyeo Makamishna
Wasaidizi Waandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) ishirini na tano (25) kuwa
Madaibu Kamishna wa Polisi (DCP) na kuwapandisha vyeo maofisa wa
Jeshi la Polisi 34 kutoka Ukamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuwa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).

No comments