Watoto na wanawake Gaza wako taabani kwa njaa huku, ukatili na kukosa huduma za msingi vikishamiri: UN
Watoto na wanawake Gaza wako taabani kwa njaa huku, ukatili na kukosa huduma za msingi vikishamiri: UN
Janga la kibinadamu huko Gaza linazidi kuwa kubwa na baya kwa kasi ya kutisha, huku mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yakionya kwamba watoto, wanawake na familia wanakabiliwa na njaa, magonjwa na ukatili wakati huduma za msingi zikisambaratika.
Kote katika Ukanda wa Gaza, watoto wengi wanaokaguliwa na timu za afya za Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA “wamearifiwa kukonda sana, kuwa dhaifu, na wako hatarini kufa iwapo hawatapata matibabu wanayohitaji kwa dharura.”
shirika hilo limesema hayo kwenye mitandao yake ya kijamii na likinukuu takwimu za Shirika la Umoja wa mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, limeongeza kuwa zaidi ya watoto 50,000 wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa Gaza tangu Oktoba 2023.
Kwa upande wke Shirika la kibinadamu la Muungano wa Ulaya Mashariki ya Kati ECHO, limesema uharibifu wa mifumo ya maji umefanya hali kuwa mbaya zaidi. Limeongeza kuwa “Kwa kuwa asilimia 60 ya miundombinu ya maji imeharibiwa na mafuta yakiwa yamewekewa vizuizi, familia hulazimika kutembea kwa saa kadhaa kutafuta maji safi”.
Ingawa msaada wa Ulaya umewezesha UNRWA kuendelea kuendesha baadhi ya visima, shirika hilo limeonya kwamba “mahitaji bado ni makubwa mno.”
Wanawake na wasichana ndio walioathirika zaidi kwa mujibu wa Shirikala Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake UN Women, likisea “milioni moja kati yao wanakabiliwa na njaa ya kutisha, ukatili na manyanyaso.”
Shirika hilo limeongeza kuwa wanawake na wasichana wamelazimika kutumia “mikakati ya hatari ya kujinusuru, ikiwemo kutoka kwenda kutafuta chakula na maji huku wakihatarisha maisha yao kwa kuuawa.”
Wahudumu wa kibinadamu wanasema hali inazidi kudorora na wanatoa wito wa kupatikana kwa furs ya haraka na isio na vizuizi ili kufikisha chakula, dawa na msaada mwingine wa kuokoa maisha Gaza.
Chanzo UN
No comments