Serikali kushirikiana na dini zote

WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inaunga mkono
dini zote nchini na kuzipa ushirikiano wa kutosha ili ziweze kufanya kazi zake
vizuri.

“Dini ndiyo inayojenga msingi imara kiroho, kiimani na ndiyo inajenga maadili
mema. Leo tunaposema kila mtu awe muadilifu tumegundua ili tufanikiwe
lazima tuweke mazingira mazuri yatakayowezesha madhehebu yote kuabudu
kwa uhuru,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi wa vijiji vya Malolo na Chimbila ‘B’ akiwa katika siku ya kwanza ya
ziara yake ya siku tatu ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Ruangwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imegundua
kuwa ili iweze kufanikiwa ni lazima ishirikian na madhehebu ya yote ili yaweze
kufanya kazi zake vizuri.

“Nikiwa mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali niliamua kuunda kamati ya
amani ya Taifa ambayo inajumuisha viongozi wa dini zote. Pia nimeiagiza
mikoa na wilaya zote kuunda kamati za amani ili kuhakikisha umoja na
maelewano miongoni mwa dini zote nchini unakuwepo,” alisema.
Alisema lengo la kamati hizo za amani ni kuhakikisha Watanzania wote
wanakuwa na maadili mema na kutambua umuhimu wa kuimarisha amani na
utulivu nchini.

Akizungumzia tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika
vijiji vya Nanganga, Nangumbu, Mbecha, Malolo, Mpumbe na Chimbila ‘B’
alisema Serikali inalifanyia kazi suala hilo.

Alisema tayari mtaalamu wa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi
ameshawasili katika wilaya hiyo na baada ya kukamilisha utafiti huo shughuli
ya uchimbaji visima itaanza.

Waziri Mkuu alisema lengo la utafiti huo ni kutaka kubaini wingi na ubora wa
maji katika eneo husika hivyo aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa na subira
wakati suala hilo likishughulikiwa.






No comments