WIKI YA MACHOZI TANZANIA,ZITTO,MWAKYEMBE WASHINDWA KUJIZUIA
| TAIFA limekumbwa na vilio na simanzi kutokana na vifo vya kufuatana vya viongozi waandamizi, akiwamo Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta na aliyekuwa Waziri wa Elimu na Ufundi, Joseph Mungai, vilivyotokea wiki hii. | ||
Sitta
alifariki dunia Novemba 7, mwaka huu, nchini Ujerumani, alipokwenda
kutibiwa katika Hospitali ya Technical University of Munich na
anatarajiwa kuzikwa leo Urambo, mkoani Tabora, huku Mungai naye
akifariki dunia Novemba 8, mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Mafinga, mkoani
Iringa.
![]() |
| Zitto Kabwe Tangulia Spika wa watu, Tangulia Spika Bunge la Wananchi Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa .. ![]() |
Baada
ya mwili wa Sitta kuagwa asubuhi katika Viwanja vya Karimjee, Dar es
Salaam jana, pia ulipelekwa kuagwa bungeni mjini Dodoma jana, huku
wabunge na wageni mbalimbali wakishindwa kujizua na kujikuta
wakibubujikwa na machozi.
Shughuli
ya kuagwa iliongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya mwili wa
Sitta kuwasili katika viwanja vya Bunge saa 8:50 mchana, ambapo wapambe
wa Bunge na maofisa wa Serikali waliokuwa wakiratibu waliuchukua saa
tisa alasiri na kuuingiza ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Viongozi
mbalimbali nao walihudhuria, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda
na mkewe, Tunu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu
mstaafu, John Malecela, wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki na wananchi
wengine walioingia bungeni kwa kibali maalumu. Baada ya mwili huo
kuwasili, Ndugai alianza kwa kuongoza shughuli hiyo kwa kuanza kwa
kuimbwa wimbo wa Taifa na baadaye kutoa salamu kutoka kwa wawakilishi wa
vyama vyote vilivyopo bungeni.
Aliyekuwa
wa kwanza kutoa hotuba alikuwa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
(ACT-Wazalendo) na alielezea namna Sitta alivyoliongoza Bunge la tisa na
kuweka misingi imara ya demokrasia kwa vyama vyote.
Alisema
Sitta anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyejaribu
kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu, shujaa wa wote wanaoamini
katika uwajibikaji wa kitaasisi, mwanasiasa aliyepanda na kushuka na
kisha kupanda na kubakia kileleni.
“Mwanamageuzi
wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania. Hata katika kifo chake, Sitta
ameweka rekodi nyingine kwa Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa
wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 – 2015, isipokuwa tu kwa kipindi
cha mwaka 1995 – 2005. Rekodi hii itaendelea kwa wengine wote
watakaofuata baada yake,” alisema Zitto na kuongeza:
“Ni
mtu wa namna gani wewe Samuel Sitta? Spika wa Kasi na Viwango,
unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya jeneza lako lililopambwa na
Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo katika nyumba
yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako
hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu (The Peoples
Speaker).
“Tuliokupenda
tunajua. Ulikuwa baba mlezi. ulikuwa mume mwema. Ulikuwa babu. Ulikuwa
kiongozi nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo.
Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa katika kukukumbuka
ewe Spika wa watu.
“Lakini
wala tunakuita Spika Sitta tu kwanini? Kwa sababu legacy yako (urithi)
ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Si kwamba umeanzisha Bunge
wewe, la hasha. Lakini ulipopokea uspika wa Bunge letu, kama ilivyo jadi
yako, uliliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha mhimili
huu na kuuweka katika nafasi yake ya Kikatiba.
“Nakumbuka
siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aongee na
baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006. Mimi nikiwa nina miaka 29 tu.
Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa
kumshawishi rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia babu, mimi
sasa alasiri, ninyi ndiyo saa nne asubuhi.”
Kutokana
na kauli hiyo, alisema Sitta anaweka misingi na kuliweka Bunge katika
nafasi yake ya kikatiba, jambo lililoendana na mabadiliko makubwa ya
Kanuni za Bunge kwa kuandikwa upya kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 2008,
ambayo pia ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo (CDCF).
Naye
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeendesha dua
kwa niaba ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), alieleza namna
alivyomfahamu Sitta na alivyomsaidia katika hatua mbalimbali za
kimaisha.
“Nasimama
mbele ya umati kushukuru kwa ajili ya Samuel Sitta kwa kumpa kipaji
kikubwa cha uongozi, ulimpa kipaji cha kuwatumikia na kuwaongoza watu
wako. Kwa uadilifu, unyenyekevu, ujasiri wa hali ya juu, ni wewe Mungu
ulimpa moyo wa kutetea wanyonge na kuwapigania na kupambana na wale wote
waporaji wa rasilimali za Taifa na kila alipopita aliacha alama za
uongozi uliotukuka na Bunge hili linashuhudia kazi aliyoifanya Sitta,
niseme nini?” alisema.
Dk. Mwakyembe aliendelea kutoa maneno yaliyowafanya wabunge na baadhi ya waombolezaji kuangua kilio.
“Tungeomba
Mungu Samuel aendelee kuwa hai lakini umempenda zaidi, umechuma ua la
uwaridi, mimi ni mmoja ya Watanzania wengi waliopendelewa na kusaidiwa
kwa kila hali na marehemu Sitta, uliyempa mkono wa kutoa moyo wenye
mapenzi ya hali ya juu,” alisema Sitta.
Pia
alisema Sitta alimfundisha siasa ambapo alimuambia: “Mdogo wangu siasa
si sayansi…kwa hiyo mdogo wangu jioteshee ngozi nene ili ukienda juu
usiathirike na joto na ukishuka chini usiathirike na baridi,” alisema
Dk. Mwakyembe.
Naye
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema kuwa
wabunge wamekutana kukumbuka mmoja wa miamba ya Tanzania.
“Ni
haki tunafanya kumbukumbu hii ndani ya ukumbi wa Bunge ambao aliutawala
kwa uhuru na uwazi. Katika historia ya Bunge nchi hii itamkumbuka kwa
uongozi wake wa miaka mitano (2005-2010) aliofanikiwa kuliondoka Bunge
katika kivuli cha utawala wa chama kimoja na kulifanya Bunge la vyama
vingi tunaloliona sasa.
“Alilifanya
Bunge kuwa lenye meno, lenye uwezo wa kuidhibiti Serikali, hii ndiyo
zawadi kubwa ya utumishi wa muda mrefu aliotuachia kama Spika kwa sababu
pia hakuwa kibaraka wa mtu yeyote.
“Alikuwa
mtu mwenye msimamo huru, hivyo tunapomkumbuka ni vema tukamkumbuka kwa
kujiuliza hili ndilo Bunge alilolitaka? Ukijiuliza utakuwa umemkumbuka
kwa namna inayostahili,” alisema Lissu.
Kwa
upande wake, Ndugai, alielezea mambo mbalimbali Sitta aliyofanikiwa
kuyabadilisha, huku akibainisha namna Mungu alivyomrudisha ili kufanya
aliyoacha.
“Hivi
karibuni niliugua sana, niliugua hadi kwa akili ya kawaida nikajiuliza
kwanini Mungu amenirudisha? Ila sasa katika maombi ya Mungu amenirudisha
ili na mimi nitende angalau aliyoyafanya Mzee Sitta,” alisema Ndugai.
Alisema
Sitta atakumbukwa kwa kulifanya Bunge la tisa kuwa la mabadiliko,
maboresho na hata kuliendesha kwa misingi ya haki, kasi na viwango.
Alisema
alikuwa mlezi wake katika nafasi mbalimbali za kuliongoza Bunge, kwa
sababu licha ya kuwa nahodha, alimpa nafasi ya kujifunza.
“Tulikuwa
wenyeviti watatu, mimi, Jenister Mhagama na Zubeir Maulid Zubeir,
ambaye sasa ni Spika wa Baraza la Wawakilishi- Zanzibar, hivyo tunaweza
kuona namna gani alivyotulea na najisikia fahari kwa fursa aliyotupatia.
“Nakumbuka
mwaka 2006 aliunda Tume ya Bunge ya kuhuisha kanuni, mimi nikiwamo,
ambapo aliwezesha kwanza wimbo wa taifa kuanza kupigwa wakati wa kuanza
Bunge na kumaliza, kuanzisha utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa
waziri mkuu, kamati za fedha kuongozwa na wapinzani ili kujenga
demokrasia.
Baada ya shughuli hiyo kukamilika Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa hoja ya kuahirisha Bunge hadi Januari 31, mwakani.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala
Bora, Angella Kairuki, alisema Taifa limempoteza Sitta, aliyekuwa
kiongozi mkubwa na shupavu aliyeweza kuandika historia yake mwenyewe
iliyosababishwa na utumishi uliotukuka.
Kairuki
alikuwa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati Sitta
akiagwa Dar es Salaam, katika shughuli iliyohudhuriwa na Rais Dk. John
Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk.
John Kijazi, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe, Salma Kikwete, Rais
mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna Mkapa, Makamu wa Rais mstaafu, Dk.
Gharib Mohamed Bilal, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji mstaafu Damian Lubuva, Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda, Spika
wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na
Jaji mstaafu Joseph Warioba.
“Aliweza
kuandika historia yake mwenyewe, watu wachache wenye uwezo huo
waliojaliwa vipawa, karama na fursa kama alivyo Sitta, kwa fikra zake,
uongozi wake na kazi za mikono yake ameweza kufanya mambo mengi yenye
manufaa kwa nchi na kutuachia alama,” alisema Kairuki.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda, alimwomba Magufuli kuwapo
kwa eneo maalumu la kuzikia viongozi waliofanya mambo makubwa katika
nchi.
“Kwa
kuwa Serikali inahamia Dodoma tunaomba kutengwe eneo, ikiwezekana la
kuzikia viongozi walioifanyia nchi mambo makubwa na hapo baadaye hata
mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tunaweza kuuhamishia
hapo,” alisema Makonda.
Makonda,
aliyekuwa akilia kwa uchungu muda wote wakati wa kuagwa mwili wa
Sitta, pia alisema atamkumbuka kwa kuwa ndiye aliyemsaidia katika kulipa
ada alipokuwa akisoma shule ya sekondari mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Sumaye, alisema Watanzania wanatakiwa kumuenzi Sitta kwa vitendo na si kwa maneno.
“Sitta
alikuwa mwadilifu, mchapakazi, mwenye busara, mpigania haki na
aliyesimamia alichokiamini, hivyo tunatakiwa tubaki navyo hivi,” alisema
Sumaye.
Naye
Msemaji wa Familia, Caroline Sitta, aliishukuru Serikali pamoja na
viongozi mbalimbali kwa kipindi chote walichokuwa wakimuuguza, huku
akisisitiza kuwa enzi za uhai wa baba yake alikuwa akipenda kusaidia
watu bila malipo.
“Kwetu
alikuwa babu, mume na baba mwenye upendo mkubwa, alipenda kusaidia watu
wapate mafanikio bila malipo, alikuwa akikumbuka siku zote za kuzaliwa
za watoto na wajukuu,” alisema Caroline.
Mbali
na kifo cha Sitta, viongozi wengine waliofariki dunia Novemba 8, mwaka
huu na kuzikwa Zanzibar ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC), Jaji Zubeir Maulid, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Salehe Ramadhan Ferouz na Mbunge wa Dimani
(CCM), Hafidh Ali Tahir, aliyefariki dunia mkoani Dodoma usiku wa
kuamkia jana na kuzikwa Zanzibar jana hiyo hiyo na kuifanya wiki hii
kuwa ngumu kwa Taifa.
Pia
watu wengine 19 walifariki dunia kutokana na ajali ya gari aina ya
Toyota Noah na lori aina scania iliyotokea usiku wa Novemba 6, mwaka huu
katika Kijiji cha Nsalala, mkoani Shinyanga.
Awali
akitoa taarifa ya msiba bungeni asubuhi jana, Ndugai, alisema Tahir
alifariki dunia kutokana na maradhi ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua.
Taarifa
hiyo aliitoa baada ya sala ya kuliombea Bunge, nchi na Rais na Ndugai
alisema Tahir amekumbwa na umauti saa nane usiku wa kuamkia jana.
“Waheshimiwa
wabunge, kuna masikitiko makubwa nawatangazia msiba wa mwenzetu Hafidh
Ali Tahir, aliugua ghafla jana (juzi) saa nane usiku na alikwenda
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na alipimwa na kubainika kuwa ana
tatizo la moyo na shinizo la damu na madaktari wakiwa wanampatia
matibabu alifariki dunia muda mfupi,” alisema Ndugai.
Baada
ya taarifa hiyo, ukimya ulitokea bungeni, huku baadhi ya wabunge
wakishindwa kujizuia na kububujikwa na machozi kutokana na msiba huo.
Licha
ya kutoa tangazo hilo, Ndugai alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini
yenye huzuni, huku kila jambo alilokuwa akiwahoji wabunge aliitikia nao
pamoja.
Ndugai alisema walikuwa na Tahir hadi juzi usiku katika kikao cha Bunge Sports Club, lakini hakuwa na dalili za kuumwa.
Pia alisema Tahir alishiriki katika semina mbalimbali na wabunge wenzake iliyofanyika New Dodoma Hotel.
“Mheshimiwa
Tahir alikuwa ni mmoja wa wabunge walioomba kwenda Urambo katika
mazishi ya Sitta, tumeondokewa na mbunge mchapakazi, mcheshi,
mwanamichezo na aliyewajali wapiga kura wake,” alisema Ndugai kwa
huzuni.
Alisema
kwa mujibu wa kanuni ya Bunge 152, inayelekeza kwa kusema kuwa
inapotokea mbunge atafariki wakati wa Bunge likiwa katika shughuli zake,
Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili maombolezo
na katika hatua nyingine, alisema nusu ya posho ya wabunge ya siku ya
jana itatolewa kama rambirambi kwa msiba wa Sitta na Tahir.
Kutokana
na hali hiyo, alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, kutengua kanuni
ili kuruhusu shughuli iliyopangwa kufanyika katika kikao maalumu cha
kumuaga Sitta na Tahir.
Pia
alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo,
Andrew Chenge, kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya utendaji kazi ya
kamati yake iliyowasilishwa juzi ili ikafanyiwe kazi na Serikali.
Baada
ya kutengua kanuni hiyo, Chenge alihitimisha kwa muda mfupi hoja yake
bila kuchangiwa na wabunge, tofauti na utaratibu mwingine unaofanyika
bungeni.
“Mheshimiwa
Spika, siku ya leo (jana) ilikuwa nzito katika historia ya Bunge letu
na haijawahi kutokea. Haijawahi kutokea mambo mazito kwa wakati mmoja
kama leo hii (jana) tunapokosea hapa na pale naomba tuvumiliane,”
alisema Chenge.
Baada
ya Chenge kumaliza kuhitimisha hoja ya kamati yake, Ndugai alisitisha
kwa kuahirisha shughuli za Bunge saa 9:30 asubuhi hadi saa 08:40 mchana
jana, ili kupata muda wa kuaga mwili wa Tahir na baadaye kuaga mwili wa
Sitta.
“Basi
tuyashike yale yanayotuunganisha zaidi, tuwe na upendo, tuwe ni watu
wenye kushirikiana. Upande wa bunge Mheshimiwa Mussa Zungu
atamuwakilisha spika na ataambatana na baadhi ya wabunge wa kutoka
Zanzibar na bara,” alisema Ndugai.
MAJALIWA
Akitoa
salamu za Serikali, Majaliwa alisema ni jambo la kushtua kwa kuwa juzi
Tahir alishiriki mambo mbalimbali ya kijamii na kibunge na enzi za uhai
wake alijali na kuthamini mchango wa wenzake.
“Leo
(jana) tunazungumza akiwa katika hali nyingine, ni jambo la huzuni
kwetu na ni funzo kwetu pia, Serikali kupitia Rais Dk. John Magufuli
inatoa salamu za pole kwa spika, wafiwa wote, wabunge tupo katika hali
ngumu, tumepoteza wabunge wenzetu tuliokuwa nao katika bunge,” alisema
Majaliwa.
Pia
aliwaasa wabunge wote kutambua safari ya kifo ni ya kila mwanadamu,
hivyo ni vyema kujenga na kuimarisha upendo miongoni mwao kwa kuishi
pamoja na kushirikiana kwa hali na mali.
“Binafsi
mimi nimemfahamu Tahir, nimewahi kuhudhuria naye kozi ya kimataifa ya
uongozi katika mchezo wa mpira wa miguu kule Zanzibar mwaka 1996,
natambua namna ambavyo alipenda majukumu yake, aliwapenda wenzake na
kushirikiana nao. Tuendelee kumuombea kila mmoja kwa dini yake,” alisema
Majaliwa.
Alisema
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi,
ndiye atakayeiwakilisha Serikali katika mazishi ya Tahir.
MBOWE
Naye
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema
msiba huo uwe somo kwa wabunge wote kwa kuwataka kupendana na
kuheshimiana.


No comments