MKURUGENZI JIJI LA ARUSHA AOMBWA KUTATUA MGOGORO

 Athuman J. Kihamia
BARAZA la Madiwani la Jiji la Arusha limemwomba Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hilo, Athumani Kihamia kuhakikisha mgogoro wa eneo la Shule ya Msingi Naura lililochukuliwa na Kikosi cha Usalama Barabarani, unatatuliwa.

Aidha, Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro alimpongeza Kihamia na wataalamu wake, kwa kujibu vyema maswali ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali mjini Dodoma.

Madiwani hao walihoji hayo juzi katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Jiji hilo, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akiuliza swali juu ya mgogoro huo jana, Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema ni kwa nini suala hilo la eneo la Shule ya Msingi Naura kuvamiwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuweka magari mbalimbali wanayoyakamata katika eneo la shule.

Pia alisema suala hilo ni la muda mrefu, lakini hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi wake hivyo ni vyema mkurugenzi wa jiji kuhakikisha anafuatilia mgogoro huo na kupata ufumbuzi ili ijulikane wazi kama ni polisi wapewe au shule.

“Mgogoro huu ni wa muda mrefu, lakini hatujui nani anapaswa kuchukua eneo lile ambalo awali lilikuwa ni la shule lakini hawa askari wamelichukua na kuweka magari wanayoyakamata, tunataka kujua lini tutaelezwa eneo hilo ni la nani,” alisema Doita.

Kihamia alisema, anafuatilia suala la mgogoro wa eneo hilo kwa kina na kikao kijacho jibu litapatikana ili kujulikana nani mmiliki wa eneo hilo.

Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Terrat, Obeid Meng'oriki alihoji jiji lina mpango gani wa kuwasaidia watumishi wanaokaa maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo ambao watapata tabu katika kutoa huduma.

No comments