RC Gambo kuanza kuwatumia viongozi wa dini kumaliza vitendo vya kihalifu Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Mashaka Gambo
amekutana na kamati ya Amani ya Mkoa ambayo inajumuisha viongozi wa
dini mbalimbali zilizoko katoka Mkoa huu kuzungumzia mustakabali wa
Amani na namna viongozi hawa wa dini watashirikiana na Serikali ya
Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo kwa wananchi ambao ni waumini
wao.
Akizungumza katika Kikao hicho Mhe. Gambo
alisema kazi ya Ulinzi wa Amani itakua rahisi sana kupitia viongozi wa
dini ambao wana karama ya kuongea na kubadilisha maisha ya watu bila
kutumia nguvu ama kuwashurutisha isipokua kwa chakula cha roho ambacho
hujenga misingi imara ya imani na tabia njema.
Maendeleo
ya wananchi hayawezi kupatikana bila Amani kuwepo katika Mkoa wetu ni
lazima tusaidiane katika hili dhamira yetu ifanikiwe kwa wepesi zaidi
tuna Imani kubwa sana Na viongozi wetu wa dini na ndio maana nikaona ni
vyema tukakutana ili tusikie kutoka kwenu ninyi ambao mnawakilisha
kundi kubwa la wananchi na pia kufahamu kero mbalimbali zinazowakwaza
wananchi katika maeneo yenu alisema Gambo.
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati KKKT Solomon Masangwa
akichangia kuhusu masuala yanayoweza kuhatarisha amani alisema kundi
ambalo linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la Tatu na litasaidia sana
katika ulinzi wa Amani ni waendesha boda boda pamoja na wanachinga ambao
kwa sasa wanaonekana kutopewa kipaumbele au hatuwajali kwa kiasi
kinachostahili.
Tunapaswa
kuangalia namna gani watu wanaofanya shughuli hizi wanakua rasmi kwa
kupatiwa maeneo maalumu pamoja na utambulisho utakaowawezesha kufanya
kazi zao kwa Amani na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na si
kama walivyo sasa wanafanya kazi hizo katika maeneo yasiyo rasmi na
kuhama kila siku hali hii ina wafanya wajihisi kama si sehemu ya Taifa
hili hivyo wanaweza kutumika kiurahisi kuhatarisha amani ya Nchi yetu
alisema Masangwa.
Akichangia katika viashiria vya uvunjifu wa amani Askofu Dr. Leornard Mwizarubi wa Kanisa la SAYUNI EAG (T)
alisema ni vyema Serikali ikajikita katika kutatua changamoto
zinazoathiri maisha ya kila siku ya wananchi ili hata sisi viongozi wa
dini tunapoongea na waumini tuwe na vielelezo dhabiti vya kuonyesha
namna ambavyo Serikali kero zao zimeshughulikiwa.
Aliendelea
kusema “Katika eneo ambalo ninatoa huduma ya Kiroho kwenye Kata za Unga
Ltd, Sokoni 1, Daraja II, Sinoni na maeneo ya jirani wakazi wa mitaa
hiyo wanapata shida sana ya huduma ya maji Taka na hata katika Kanisa
langu inanilazimu kutafuta gari la kunyonya maji taka mara tatu kwa wiki
ili kufanya mazingira kuwa safi, sasa kuna maeneo mengine wananchi hao
hawana uwezo wa kutafuta gari hilo la kunyonya maji taka hivyo wanaishia
kulalamika kwa kuishi katika mazingira machafu”.
Aidha Sheikh Mkuu wa Bakwata mkoa wa Arusha, Shabaan Juma alishkuru
Sekretariet ya Mkoa kwa kikao hiki muhimu kwa ustawi wa jamii ya Arusha
na kueleza kuwa katika kipindi hiki cha Mpito Nchi yetu inahitaji
maombi ya bila kikomo ili kuweza kuvuka salama na tunategemea kuendelea
kuona mabadiliko katika kila eneo; Tunaamini si wote wanafurahia
mabadiliko haya hivyo tuna wajibu wa kuwajulisha waumini wetu kuhusu
umuhimu wa mabadiliko ya mifumo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya
Tano na faida zitakazo patikana kwa Taifa.
Akiwasilisha
changamoto katika upande wake Sheikh Shaaban alisema “Kuna ukuaji wa
kasi ya makazi holela katika Jiji la Arusha, Utaratibu wa mipango miji
hauzingatiwi na hii inasabisha maeneo mengi kutopitika kwa urahisi
hivyo hata itakapotokea dharua sio tahisi kwa wananchi wetu kupata
msaada wa haraka, tunaomba wanachi wapimiwe maeneo yao, barabara
zifunguliwe ili huduma muhimu ziweze kufika katika maeneo hayo”.
Mkurugenzi
wa Idara ya maji safi na maji Taka (AUWASA) Eng. Ruth Koya alisema
Taasisi yake inaanza utekelezaji wa Mradi mkubwa wa maji safi na Taka
ambao matatizo yote yaliyowasilishwa katika kikao hiki yanayohusiana na
maji yatashughuliwa kupitia mradi huo.
Aliongeza
kuwa mradi huo utahusisha uboreshaji wa mioundombinu ya maji safi,
Uhamishaji wa mabwawa ya maji Taka(yaliyokuwa Lemara kwa hivi sasa),
ununuzi wa magari ya kunyonyea maji machafu pamoja na magari ya
kusambaza na kuuza maji safi.
Mkuu wa
Mkoa Mge. Gambo alitolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizowasilishwa
na kuelezea namna ambavyo Changamoto ya Mipango Miji ilivyopata ufumbuzi
kupitia ukamilishaji wa Mpango Mkakati wa Jiji la Arusha (Master Plan)
na kuwajulisha wajumbe kuwa mpango umekamilisha na umekwishapitiwa na
Halmashauri zote tatu zinazohusika, hivyo kwa hivi sasa utawasilishwa
Wizarani na taratibu zote zikikamilika utekelezaji utaanza mara moja.
Kuhusu
suala la Machinga na waendesha bodaboda Rc Gambo alisema Serikali
imekwisha anza utaratibu wa kutafuta maeneo salama na rafiki kwa ajili
ya wafanyabishara ndogondogo maarufu kama machinga na tutaongea nao ili
tuwe na makubalino ya pamoja.
Aidha
kuhusu bodaboda tumeanza kuwatambua kupitia kwenye uongozi wa mitaa na
vituo vyao na tutahakikisha tunaboresha mazingira yoa ya kufanyia kazi
na zaidi tunawatafutia Pikipiki ambazo watapewa Vijana wanaofanya
biashara ya boda boda kwa utaratibu maalumu; Itawapasa kurudisha Fedha
za Pikipiki tu na kisha kupata umiliki halali ya Chombo hicho tofauti na
sasa hivi ambapo wanapewa pikipiki hizo na kulipa mara mbili ya bei kwa
matajiri wao ndipo wapate Umiliki alimalizia Gambo.
Na Nteghenjwa Hosseah – Arusha
No comments