Rais Magufuli amlilia Mungai, Sumaye, Warioba wamchunia Mkapa


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli leo kwa huzuni amewaongoza mamia ya watu kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Serikali ya awamu ya tatu Joseph Mungai katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
 
Miongoni mwa viongozi wastaafu waliohudhuria sherehe ya kuuaga mwili wa Mungai ni rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Jaji Mkuu mstaafu Joseph Warioba na aliyekuwa waziri mkuu wa awamu ya tatu Fredrick Sumaye.

Hata hivyo, Warioba na Sumaye walipoingia ukumbini hawakutoa mkono wa salamu kwa Mkapa kitendo kilichoshangaza baadhi ya watu.

Msemaji kwa niaba ya serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Augustine Mahiga amesema serikali imepoteza mtu wa muhimu kutoka na uchapakazi wake sambamba na mchango wake katika maendeleo ya taifa hasa kwenye sekta ya kilimo na elimu.

Mungai aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo katika serikali ya awamu ya kwanza na nne pamoja na waziri wa elimu wa awamu ya tatu alifariki dunia ghafla Novemba 8, 2016 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokua akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa wasifu wa Mungai enzi za uhai wake uliosomwa na mwanae Jimmy Mungai, ameacha mke mmoja na watoto 7.
Mazishi yatafanyika siku ya Jumamosi Mafinga mkoani Iringa.

No comments