Balozi Seif Ali Iddi aongoza Kikao cha Mawaziri, Manaibu Mawazini na Makatibu Wakuu wa SMZ
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Wizara za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mawaziri, Watendaji Wakuu
pamoja na Wataalamu wao kufanya uchambuzi wa kuorodhesha mambo ambayo
yanaonekana kuleta changamoto kuhusu kero za Muungano.
Alisema
orodha ya uchambuzi huo katika kila Sekta baadaye unapaswa kuwasilishwa
katika Kamati ya Sekriterieti ya Vikao hivyo iliyo chini ya Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akikiongoza Kikao cha Mawaziri,
Manaibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara za SMZ
kilichofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kupokea mambo ambayo
tayari yamekubalika kutekelezwa katika Vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT
na SMZ kuhusu kero za Muungano.
Alisema
kazi iliyopo hivi sasa kwa Watendaji wa Kamati hiyo ya pamoja kwa
upande wa Zanzibar ni kukumbushana kwa nia ya kutafuta mapungufu
yaliyojitokeza ndani ya utekelezaji wa kero za Muungano hasa
ikizingatiwa zaidi mabadiliko ya Uongozi yaliyojitokeza ndani ya
Wizara za Serikali.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed
Aboud Mohammed alieleza kwamba suala lolote wanalolihisi Mawaziri hao
linafaa kuwa agenda ni vyema likawasilishwa mapema kwenye Kamati ya
Sekriterieti.
Waziri
Aboud alisema hatua hiyo itawapa fursa Watendaji wa Sekriteriet hiyo
kuyapitia masuala hayo na kuyapa upendeleo wa kuingizwa katika agenda za
Vikao vinavyotarajiwa kushirikisha Wajumbe wa Kamati ya Pamoja na pande
hizo mbili.
Mapema
akitoa Taarifa ya Kikao hicho Katibu wa Kamati ya Sekriteriet ya Kero
za Muungamo ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza alisema Kamati hiyo tayari imeshafanya
tathmini ya vikao vilivyopita.
Katibu
Mkuu Meza alisema uchambuzi wa tathmini hiyo utaweza kuwasaidia Wajumbe
wapya wa Kamati hiyo katika kujadili kwa kina masuala yanayohusu
Changamoto za Muungano.
Wakichangia
agenda hizo baadhi ya Washiriki wa Kikao hicho walipendekeza kuwepo kwa
uelewa wa pamoja wa Washiriki hao katika kujadili masuala ya changamoto
za Muungano ambao ndio njia rahisi ya upatikanaji wa ufanisi wa haraka.
Kikao
cha Mwisho cha Kamati ya pamoja ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar cha kujadili Kero za Muungano chini ya Mwenyekiti wake Makamu
wa Rais wa Muungano kilifanyika Mjini Dodoma Mnamo Tarehe 23 Juni mwaka
2013.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao cha
Mawaziri, Manaibu Mawazini na Makatibu Wakuu wa SMZ kupokea mambo na
utekelezaji wake yaliyokubalika kutekelezwa katika Vikao vya Kamati ya
pamoja ya SMT na SMZ kuhusu kero za Muungano.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla
Meza akiwasilisha Taarifa kwenye Kikao cha Mawaziri, Manaibu Mawazini na
Makatibu Wakuu wa SMZ kuhusu kero za Muungano.
Baadhi
ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za SMZ wakiwa
katika Kikao cha kupokea mambo na utekelezaji wake yaliyokubalika
kutekelezwa katika Vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ kuhusu kero
za Muungano. Picha na OMPR – ZNZ.



No comments