AJALI YA NOAH,LORI ILIYOUA 19 SHINYANGA YANG’OA VIGOGO WA POLISI.
Uamuzi huo umetolewa leo na kaimu kamanda wa kikosi cha usalama
barabarani nchini SACP Fortunatus Muslimu wakati akitoa taarifa kwa
vyombo vya habari mkoa wa Shinyanga kuhusu hatua zilizochukuliwa na
jeshi la polisi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
“Noah ilianza safari katika kituo cha Nzega majira ya saa 12:30 jioni
Novemba 06,2016, ikiwa na abiria 17 kati yao watu wazima 13 na watoto
wanne waliokuwa wamepakatwa na wazazi wao ...wakati gari linaondoka
askari waliopangwa kazini eneo hilo walikuwa wameshaondoka
kituoni...,gari hilo halikukaguliwa hivyo kutoa mwanya kwa gari hilo
kubeba abiria kupita kiasi kwa kuzidisha abiria”,ameeleza Muslimu.
Amesema kitendo cha askari kuondoka eneo la
tukio,kilifanya gari izidishe abiria watano watu wazima na watoto wanne kwani
Noah inapaswa kubeba abiria wanane (8) na si vinginevyo kwa mujibu wa sheria.
Amebainisha kuwa vile vile askari waliopangwa kazini barabarani eneo la Uchama- Nzega nao
walikuwa wameondoka eneo hilo hivyo
kutoa mwanya mwingine wa gari hilo kubeba abiria wengine wanne njiani eneo la
Nata ambapo inadaiwa kulikuwa na basi lilikuwa limeharibika na abiria kusimamisha
Noah.
“Noah ilisimama
na abiria kulazimisha kupanda ndani ya gari hilo na hivyo kuongeza idadi ya
abiria katika gari hilo kufikia jumla ya watu 21 pamoja na dereva na hivyo
ndani ya Noah kuwa na watu 22 na dereva akaendesha gari kwa mwendo kasi bila
kuchukua tahadhali na kasha kugongana na lori”,ameongeza Muslimu.
Amesema ajali hiyo imechangiwa na uzembe wa askari hivyo mkuu wa usalama
barabarani wa wilaya ya Nzega Thomas Sengecha na mkuu wa usalama
barabarani mkoa wa Tabora Shida Machumu wanavuliwa nyadhifa zao kwa
kushindwa kutekeleza mkakati wa kupunguza ajali na kushindwa kusimamia
na kuchukua hatua kwa watendaji walio chini yao.
Mbali na kuvuliwa nyadhifa zao pia wanaondolewa katika kikosi cha usalama barabarani na watapangiwa kazi nyingine.

No comments