Godbless Lema Arudishwa Rumande Baada ya Kunyimwa Dhamana Kwa Mara ya Pili
Ujanja
wa kisheria uliosababisha mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kukaa
mahakamani kwa saa 10, umemfanya kada huyo wa Chadema kukosa tena
dhamana.
Jana,
Mahakama ya Hakimu Mkazi ilishatupilia mbali hoja za Serikali za
kupinga dhamana ya mbunge huyo, lakini mawakili walitumia silaha
nyingine ya kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa kumpa dhamana
Lema.
Mawakili
wa Serikali walifanya hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha kutupa hoja za kuzuia
dhamana ya Lema na hivyo kumzuia hakimu kuendelea na utaratibu wa
kumwachia mbunge huyo kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo, hali iliyoibua
vilio mahakamani.
Kutokana na maamuzi hayo, hatma ya Lema kupata dhamana inasubiri Mahakama Kuu kupanga jaji wa kusikiliza shauri hilo.
Lema,
ambaye alifikishwa mahakamani saa 2:00 asubuhi, alirudishwa mahabusu
akiwa kwenye basi la magereza lililokuwa na ulinzi mkali saa 11:00
jioni.
Katika
uamuzi wake uliotupilia hoja za awali za Serikali kupinga dhamana,
Hakimu Kamugisha alisoma maamuzi kwa saa 2:35 na kutoa dhamana kwa Lema.
Hakimu
Kamugisha alisema upande wa mashtaka uliwasilisha hoja tatu za kupinga
dhamana ya Lema katika kesi za uchochezi namba 440 na 441/2016 na hati
ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha(RCO).
Alisema
hoja ni kuwa mshtakiwa ametenda makosa hayo, wakati akiwa nje kwa
dhamana kwa kesi namba 351 na 352 za mwaka 2016, jambo ambalo ni kinyume
cha sheria.
Hakimu
Kamugisha alisema hoja nyingine ni kutaka Lema anyimwe dhamana kwa
ajili ya kulinda usalama wake, hasa kwa kuwa kauli zake za uchochezi
dhidi ya Rais John Magufuli zimewaudhi wananchi.
Hoja ya tatu kujali maslahi ya Taifa. Hoja hizo ziliandamana na hati hiyo ya kiapo cha RCO.
Hata
hivyo, hakimu alisema mawakili wa utetezi waliokuwa wanaongozwa na John
Mallya walipinga hoja hizo, wakisema dhamana ni haki ya mshitakiwa na
kuwa nje kwa dhamana katika mashauri mengine ambayo hayajamtia hatiani
mtuhumiwa, hayawezi kuwa sababu ya kumnyima dhamana.
Alisema
mawakili hao, pia walipinga hoja za kutokutolewa dhamana kutokana na
usalama wake na maslahi ya Jamhuri na pia wakakosoa hati ya kiapo kuwa
ina mapungufu, hasa ya kutokuwa na uthibitisho wa mambo yaliyoelezwa.
Hakimu Kamugisha alisema msingi wa haki ya dhamana ni wa Katiba ibara ya 15(1) na (2) ambayo inaelezea uhuru wa mtu.
Alisema
pia ibara ya 17 ya Katiba inatoa haki ya mtu kutembea popote na
kuongeza ibara ya 16(6) B inaeleza mahakama inamchukulia mtuhumiwa
yeyote kuwa hajafanya kosa hadi anakapotiwa hatiani.
Alisema washitakiwa hupelekwa mahabusu ili iwe lazima mtuhumiwa kufika mahakamani.
Hakimu
Kamugisha alisema, siku zote dhamana haitolewi ikiwa tu kuna mazingira
ya kisheria ambayo yameelezwa na kuwekewa masharti na utaratibu wake.
Alitolea
mfano kesi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) dhidi ya Daudi Beda ambapo
ilielezwa haki za mshtakiwa na sababu ambazo zinaweza kuzuia dhamana.
Alisema
katika kesi hiyo, mahakama iliamua kuwa ili kunyimwa dhamana lazima
kuwepo mazingira yaliyoanishwa kisheria na utaratibu ulioanishwa
kisheria.
“Nimeshindwa
kupata kifungu chochote cha sheria ambacho kinazuia kutoa dhamana kwa
mtuhumiwa aliye nje kwa dhamana ambaye ametenda makosa mengine ambayo
hayahusiani na masharti ya dhamana ya awali,” alisema.
Alisema
hata maelezo kuwa watu waliohudhuria mkutano hawakuridhishwa na kauli
za Lema na kwenda kulalamika kwa RCO, hayana panapoonyesha usalama wa
mtuhumiwa upo mashakani.
Alisema
ili hoja ya dhamana izuiwe kwa maslahi ya Jamhuri, inakuwa na hati ya
maombi hayo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) na si RCO hivyo
haoni msingi wa kutotoa dhamana hiyo “Hivyo kwa uchambuzi huu wa
kisheria natoa dhamana kwa mshitakiwa,” alisema.
Hata
hivyo, wakati anajiandaa kuandika masharti ya dhamana, ndipo wakili
mwandamizi wa Serikali, Paul Kadoshi aliwasilisha notisi za kupinga
uamuzi wa dhamana hiyo.
Alisema
anawasilisha notisi hiyo chini ya kifungu cha 379 (1) cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya mwaka 2002.
Alisema nia ya kuwasilisha notisi hiyo inatokana na mabadiliko ya Sheria za Makosa ya Jinai namba 27 ya mwaka 2008.
Alisema
kifungu cha 31 aya G katika sheria hiyo kifungu 379(1 ) (a) kwa
kuongeza maneno kuwa notisi ya kukata rufaa inaweza kujulikana kama ni
rufaa.
Alisema
mabadiliko ya sheria hiyo yalimpa hadhi DPP anapoeleza notisi ya rufani
kuwa tayari ni rufani kamili na hivyo notisi hiyo ikitolewa mwenendo wa
kesi nzima unapaswa kusimama.
Kadoshi
alisema maamuzi hayo, yamefikiwa katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Harry
Kitillya na wenzake wawili, pale DPP alipowasilisha notisi na rufani na
kesi kusimama.
Hata
hivyo, licha ya mawakili wa utetezi, Sheki Mfinanga na Richard Shediel
kupinga hoja hiyo, Haklimu Kamugisha, ambaye aliomba dakika 10
kutafakari suala hilo, alikubaliana na hoja za upande wa Serikali za
kumkatalia Lema dhamana.
Kutokana
na maamuzi hayo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema
chama hicho kimewataka wanasheria wake, Tundu Lissu na Peter Kibatala
kwenda Arusha kuongeza nguvu katika kudai haki ya Lema kuwa huru.
Mke wa Lema, Neema Lema aliwataka wakazi wa Arusha kuwa watulivu, akisema mbunge huyo anapigania uhuru wa wananchi.

No comments