Tuesday, May 3, 2016 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo 'Ageuka Mbogo' Baada ya Kukabidhi Zawadi HEWA Mei Mosi
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ameagiza ifikapo leo, wakurugenzi
wa halmashauri za mkoa huo, wawe wamewapa zawadi zao watumishi bora wa
mwaka huu baada ya kubaini walitoa zawadi hewa kwenye sherehe za Mei
Mosi.
Ameagiza pia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani pamoja na mkurugenzi wa
Shirika la Elimu Kibaha, nao kutoa zawadi ya fedha kwa wafanyakazi
waliofanya vizuri kwenye vitengo vyao, badala ya kuwapa vyeti pekee.
Akizungumza juzi kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kimkoa wilayani
Mkuranga, Ndikilo alitoa siku tatu zinazoisha leo, taasisi hizo ziwe zimetekeleza
agizo hilo. Alisema walichofanya ni masihara na yeye hayuko tayari kufanyiwa
mzaha katika suala hilo, lililoandaliwa kwa muda mrefu.
“Katika risala ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA)
Mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri
kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri kama motisha,”
alisema
Aliendelea, “Lakini kwa hali hii siwezi kukubaliana nalo, nawapa siku tatu muwe
mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini kwangu
akutane na adhabu niliyoiandaa.”
Alisema hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo
mazito na kwamba atachukua hatua kali kwa halmashauri ambazo zitashindwa
kutoa zawadi hizo kwani zingine zimetoa kwa nini wengine washindwe.
“Mimi siyo mtani wenu, wala si saizi yenu, haiwezekani mniite nije kutoa
zawadi hewa, ndo maana hatua zikichukuliwa za kinidhamu mnasema
mnaonewa, ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika, huu ni
mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema
Ndikilo.
Licha ya ofisi ya Katibu Tawala pamoja na Shirika la Elimu Kibaha, taasisi
nyingine zilizotakiwa kutekeleza agizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo,
Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji .
“Hatutaniani hapa,huu ni mzaha uliopitiliza kiwango,.ujumbe umefika.Namna hii
mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni jambo ambalo
halijanifurahisha na nisingependa hali hii ijitokeze tena,” alisema Ndikilo.
Awali, akisoma risala ya Tucta, Amini Msambwa alisema kuwa wafanyakazi
wana haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima zipatikane kwa
shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje waajiri.
Msambwa alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa nje
na wa ndani, kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao sehemu za
kazi, ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka
huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za wafanyakazi.
No comments