Mbowe: Edward Lowassa na Fredrick Sumaye,Watajwa katika sakata la uuzaji nyumba za serikali.


Uuzwaji wa nyumba za serikali umegeuka mwiba huku wabunge wakiendelea
kuhoji hatua zilizochukuliwa kutokana na kadhia hiyo
Hatua hiyo iliyotekelezwa mwaka 2002 hadi 2004 ilizusha malalamiko mengi
tangu wakati huo na sasa imeibuka tena bungeni

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano
jana, mbunge wa Nachingwea, Hassani Masala (CCM) alihoji mfumo uliotumika
kuuza nyumba za serikali
Alisema haungi mkono kwa vile umesababisha viongozi wapya wa serikali
wanaoteuliwa kujikuta wakiishi katika nyumba za wageni.

Mjadala huo uliibuliwa juzi na msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni kupitia
kwa waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema kabla
ya Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan Zungu kumtaka kuondoa baadhi ya
maneno katika hotuba yake likiweo suala la uuzwaji wa nyumba za serikali.
Ritha Kabati Amvaa Lowassa

Akichangia mjadala huo jana, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati
alimtaja aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa kuwa alinunua nyumba ya serikali iliyouzwa
mwaka 2002 yenye jengo namba 68.

Alisema hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisema nyumba za
serikali 7,921 ziliuzwa tangu mwaka 2002 hadi 2004 na kutaka serikali ya
awamu ya tano kurejesha nyumba hizo kutokana na walionunua kukiuka
mikataba na malengo ya mauzo.

“Naomba niwaambie usiangalie boriti lililo katika jicho la mwenzako wakati
kwako lipo, kwani hata mgombea wao wa urais Edward Lowassa alihusika kwa
kununua nyumba ya plot namba 68 na Fredrick Sumaye alikuwa Waziri Mkuu
na kuhusika kuuza nyumba hizo,” alisema Kabati.

Baada ya kueleza hayo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliomba kumpa taarifa mbunge
huyo kuwa taarifa hiyo ni kwa maslahi ya taifa, hata kama mhusika atakuwa
katokea kambi ya upinzani sheria itachukua hatua.

"Kambi ya upinzani tunapoibua jambo huwa linakuwa kwa maslahi ya Taifa,
hivyo ni vyema wabunge wote mtambue kuwa kosa likifanywa na kiongozi ni
lazima hatua zichukuliwe bila kujali ni wa Chadema, CUF au CCM.

"Tunapokuwa tunatoa uamuzi kama kambi ina maana sheria ifuate mkondo
wake." Alisema Mbowe huku akishangiliwa na wabunge wa UKAWA
Awali katika michango mbalimbali ya wabunge wa upinzani wamekuwa
wakilalamikia kuuzwa nyumba hizo za serikali na kudai kuwa watumishi wapya
wengi walioajiriwa, wamekuwa wakikosa maeneo ya kuishi.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) akichangia mjadala huo alilalamikia
kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na nyingine za Tazara zipatazo 500 na
kuamua kumpatia Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ripoti aliyodai
inaonesha nyumba hizo zilivyouzwa.
l

No comments