MHIFADHI MWANDAMIZI WA TANAPA ASHIKILIWA NA KIKOSI KAZI MAALUM CHA KUPAMBANA NA UJANGILI NCHINI.


KUSHIKILIWA NA KIKOSI KAZI MAALUM CHA KUPAMBANA NA
UJANGILI KWA MHIFADHI MWANDAMIZI GENES SHAYO.

Mhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Genes Shayo (60)
anashikiliwa na Kikosi Kazi Maalum cha kupambana na ujangili nchini
kufuatia taarifa za kuhusishwa kwake na upatikanaji wa jino la
tembo wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Shirika la Hifadhi za Taifa kupitia taratibu za utendaji kazi lilipokea
taarifa za kintelijensia tarehe 14.05.2016 zikimhusisha mwananchi
mmoja mkazi wa Ngarenanyuki, Arumeru Emmanuel Nassari (46)
ambaye ni Mchungaji wa Kanisa TAG kumiliki jino la tembo na kuwa
alihitaji kupata mtu wa kufanya naye biashara. Baaada ya kupata
taarifa hizi shirika liliwasiliana na Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa
kinachohusika na masuala ya ujangili ili kushirikiana kwa ajili ya
ufuatiliaji.

Kikosi Kazi hiki mara baada ya kupata taarifa hizi kiliendelea na
taratibu zake za kiuchunguzi na baada ya ufuatiliaji walifanikiwa
kumkamata Emmanuel Nassari tarehe 15.05.2016 akiwa na jino moja la
tembo ambapo katika mahojiano yaliyofanyika alimhusisha Mhifadhi
Mwandamizi wa TANAPA Genes Shayo kuwa anazo taarifa za yeye
kuwa na jino hilo na hivyo kukamatwa tarehe 16.05.2016 kwa ajili ya
mahojiano zaidi.

Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutoa wito kwa raia wema wa
nchi hii kuendelea kutoa taarifa za kufichua vitendo vya ujangili na
kwamba halitasita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote anayehusika na
vitendo hivi ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake watakaobainika
kisheria kuhusika na vitendo hivi.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
Simu: +255 027 254 4082
Baruapepe: dg@tanzaniapaks.go.tz
Wavuti: www.tanzaniaparks.go.tz 

No comments