Rais Magufuli Awasili Nchini Uganda LeoKuhudhuria Sherehe Za Kuapishwa RaisMuseveni





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 11 Mei, 2016 amewasili Jijini Kampala nchini Uganda ambapo kesho
anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya
Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni.

Rais Magufuli ametua katika uwanja wa ndege wa Entebe majira ya saa tano za
asubuhi na kupokelewa na Waziri wa Ujenzi na usafirishaji wa Uganda
Mheshimiwa John Byabagambi na kisha kuelekea Ikulu ya Entebe ambako
amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta
Museveni

Akiwa katika Ikulu ya Entebe Rais Magufuli amekagua gwaride rasmi
lililoandaliwa kwa heshima yake na pia amepigiwa mizinga 21.
Aidha, Viongozi hao wamefanya mazungumzo ambapo pamoja na kujadili
masuala mbalimbali ya ushirikiano na uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Rais
Magufuli amemhakikishia Rais Museveni kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa
kutosha kufanikisha ujenzi wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka
Hoima katika Ziwa Albert nchini Uganda na kupita kaskazini mwa Tanzania hadi
bandari ya Tanga.

Rais Magufuli ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kampala
11 Mei, 2016
RAIS

No comments