Bodi ya Filamu yasitisha usambazaji wa Filamu ya “Imebuma”

Bodi ya Filamu Tanzania imesitisha usambazaji wa filamu ya “Imebuma” mpaka
pale maudhui yake yatakapofanyiwa marekebisho.

Akisitisha usambazaji wa filamu hiyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu
Tanzania Bi Joyce Fisso amesema mtengenezaji wa filamu hiyo hana kibali cha
kutengenza filamu kutoka Bodi ya Filamu na hajazingatia Sheria na kanuni za
utengenezaji wa filamu.

Bi Joyce Fisso amesema filamu hiyo imesitishwa kwenda sokoni kutokana na
kukiuka vifungu vya kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya
mwaka 2011 ambayo inakataza kuonesha namna yoyote ya udhalilishaji wa
kibinadamu katika filamu na maigizo.

“Baada ya kuangalia kwa makini filamu hii na kuona mapungufu ambayo
yanakinzana na Kanuni za Sheria ya filamu na Michezo ya kuigiza nimeamua
kuisitisha usambazaji wake mpaka pale wahusika watakaporekebisha maudhi
yake” Alisema Bi Joyce.

Bi Joyce amefafanua kuwa filamu hiyo imeonesha baadhi ya matukio ya
udhalilishaji wa kibinadamu, ushawishi wa matendo ya ngono na ushoga
ambayo ni kinyume na madili ya mtanzania.

Aidha kwa upande wake Afisa Utamaduni kutoka Bodi ya Filamu Tanzania Bw.
Julius Tairo amewataka waandaaji na waigizaji wa filamu nchini kufanya utafiti
wa kutosha kuhusu maudhui ya filamu kabla ya kutengeneza ili kuondokana na
utengenezaji wa filamu zisizofata Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu
Tanzania.

No comments