Vigogo Chadema Kyela Wavuliwa Uongozi kwa Usaliti


Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Saadati Mwambungu pamoja
na wajumbe 19 wa kamati ya utendaji wa wilaya hiyo, wamevuliwa uongozi
baada ya kutuhumiwa kukihujumu chama.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi jioni na uongozi wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini, chini ya mwenyekiti wake, Dk Stephen Kimondo na Mratibu wa Kanda,
Frank Mwaisumbe na kuweka wilaya hiyo chini ya uangalizi wa uongozi wa
Mkoa wa Mbeya ndani ya siku 30 wakati wakiendelea na uchunguzi.
Mratibu wa Chadema katika Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema jana kuwa
baada ya kufanyia kazi tuhuma 17 zilizowasilishwa kwao na wanachama wa
chama hicho wilaya, walibaini kuwa tuhuma saba kati yake zina ukweli dhidi ya
viongozi hao hivyo wakafikia uamuzi wa kuwasimamisha na kuwataka
kurudisha mali zote za chama hicho ndani ya siku 30.
“Ni kweli jana (juzi) tulifika Kyela na katika kikao chetu na kamati ya utendaji
ya wilaya tulipowahoji ilionekana tuhuma saba zina ukweli na baadhi ya
watuhumiwa walikiri. Miongoni mwa tuhuma hizo ni matumizi mabaya ya fedha
na mali za chama, kutoshiriki vyema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hadi
tukapoteza jimbo, hususani siku ya kuhesabu kura za jumla viongozi
walikimbia.
“Siku ile ya uchaguzi wa mwaka jana kuna vijana wetu walikamatwa
wakituhumiwa kuvunja ofisi pale halmashauri ya Kyela na wakahukumiwa, lakini
hakuna kiongozi yeyote ngazi ya wilaya aliyethubutu hata kwenda kuwaona pale
gerezani hadi walipojinasua wenyewe,” alisema Mwaisumbe.
Alisema kutokana na mkutano wao wa juzi wajumbe wake kutotimia ili kufikia
uamuzi halali wa kuwachukulia hatua zaidi, uongozi wa Kanda uliamua
kuwasimamisha na chama kuwa chini ya mkoa, huku ukifanyika utaratibu wa
kuitisha mkutano mkuu ambao utawajadili kwa kina na kuona kama
watafukuzwa moja kwa moja au la.
Mwambungu alipoulizwa juu ya kutimuliwa kwao, alikiri huku akisisitiza kwamba
tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote kikatiba, na badala yake
zimetengenezwa na ‘genge’ la watu wachache kwa uchu wa madaraka, lakini
hana kinyongo kusimamishwa uongozi kwa kuwa ipo kikatiba ndani ya
Chadema.
Alisema; “Kwanza ni heshima kwa kuwa jambo hili lipo kikatiba. Lakini katika
mkutano wa juzi akidi ya wajumbe haikutimia kwani Chadema Wilaya ya Kyela
ina wajumbe 349 wa mkutano mkuu, lakini kwa juzi wajumbe waliohudhuria
walikuwa 120 tu.
“Ndiyo maana uongozi wa Kanda ulitoa siku 30 za kufanyika mkutano mkuu
utakaowajumuisha wajumbe wote 349 na ndipo itakapofahamika… kama ni
kufukuzwa au kuendelea na uongozi,” alisema.
Mwambungu alisema kati ya wajumbe 19 wa kamati ya utendaji ya wilaya,
wajumbe saba waliamua kujiuzulu uongozi na baadaye wakaungana na wengine
ambao waliunda tuhuma hizo kwa lengo na kuuangusha uongozi ikiwa ni
maandalizi ya uchaguzi mwaka 2020.

No comments