MWENYEKITI WA MTAA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MWANZA



MWENYEKITI wa Mtaa wa Bulale wilaya ya Nyamagana mkoani
Mwanza, Alphonce Nyinzi (48) ameuawa kwa kupigwa risasi na
watu wasiofahamika wakati akielekea nyumbani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mwanza, SACP Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo
lilitokea Aprili 22 mwaka huu majira ya saa 2 usiku.

Msangi amesema kuwa marehemu aliekuwa akifahamika kwa
jina maarufu "msukuma" mfanyabiashara na mkazi wa bulale
aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na kutokea chini ya kwapa
upande wa kulia na watu wawili wasio fahamika pamoja na
risasi hiyo kumjeruhi Neema Marangula (23) Mkazi wa Bulale
katika Kiganja cha mkono wa kulia.

Amesema kuwa wakati Mwenyekiti huyo akitoka kwenye kikao
alichofanya na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa
Mtaa wa Bulale akiongozana na wajumbe wawili alikutana na
Neema Marangula akiwa na mume wake ambao walikua
wanawafuata marehemu na Balozi kwa ajili ya kuzungumzia
mzozo wa ndani ya ndoa yao kwa hiyo walikua wanahitaji
kusuluhishwa.

Mwenyekiti huyo (marehemu) na wajumbe wake wawili wakiwa
pamoja na Neema pamoja na mumewe wakiwa wanajadili tatizo
hilo hapo barabarani mara ghafla wakatokea watu wawili ambao
walikua wakipita barabarani na kuwaambia mko chini ya ulinzi
na mmoja wao akatoa bunduki na kumpiga risasi mwenyekiti
huyo ambaye alianguka chini huku wenzake wakikimbia
kujiokoa kutoka eneo hilo lakini pia wale wahalifu wakakimbia
na kutokomea gizani vichakani.

Amesema wananchi wa eneo hilo ambapo mwenyekiti aliuawa
walijitokeza kwa msaada wa kumsaidia walimchukua na
kumkimbiza hospitali kwa matibabu lakini alifariki dunia
wakiwa njiani. majeruhi Neema Marangula amelazwa Hospitali
ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa matibabu na hali yake
inaendelea vizuri.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Mkoa wa
Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi wa daktari, chanzo
cha mauaji hayo bado hakijafahamika pamoja na uchunguzi
tukio hilo bado unaendelea.

Msangi amewaomba wananchi wenye taarifa zozote kuhusiana
na tukio hilo zitakazo saidia kufanikisha kukamata wahusika
wazitoe polisi lakini pia kutoa ushirikiano kwa viongozi wao na
kuhakikisha wanatengeneza makazi salama huko wanapoishi na
maeneo ya shughuli zao na msako mkali unafanyika na
kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwada.

No comments