Waziri Masauni:Magari ya Washawasha Kugeuzwa ya Zimamoto.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusufu Hamad Masauni, amesema
Serikali iko katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kubadili matumizi
magari ya polisi ya kuzuia ghasia kwa kurusha maji ya kuwasha maarufu
washawasha yaweze kutumika kuzima moto.
Kauli hiyo ilitokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Mbozi (Chadema),
Pascal Haonga aliyeuliza ni kwanini Serikali inanunua magari ya washawasha
yasiyo na tija ambayo hutumika nyakati za uchaguzi tu badala ya kununua
magari ya zimamoto.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Masauni alisema magari ya washawasha bado
yana tija kwani Serikali inafanya taratibu ili magari hayo yatumike kuzima moto
kwenye majanga na isiwe kwa washawasha pekee na kuwataka wabunge hasa
wa upinzani kuondoa fikra za kuyapinga magari ya washawasha kwani sasa
itakuwa ni neema kwao badala ya kutumika kwa kudhibiti vurugu pekee.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana Serikali ilinunua magari ya
washawasha 777 kwa bei ya kati ya Sh150 milioni na Sh400 milioni, hata hivyo
taarifa zingine zilisema magari yaliyotumika wakati wa uchaguzi ni 50.
Awali Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), aliuliza swali la
msingi kwamba ni lini Serikali itapeleka huduma ya zimamoto katika mpaka wa
Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya
moto inapotokea.
Naibu Waziri Masauni alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika halmashauri
ya Mji wa Tunduma lina kituo katika eneo la mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya
Momba katika Mkoa wa Songwe, kinachohudumia wilaya yote ukiwamo mpaka
huo.
Alisema kwa sasa kituo hicho kina gari moja ambalo nalo liko kwenye
matengenezo mjini Mbeya likiendelea kufanya matengenezo huku askari
wakiendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na majanga ya moto.
Masauni alisema ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya zimamoto katika
maeneo ya nchi ikiwamo Tunduma, mpango huo unategemea upatikanaji wa
fedha kwa Serikali.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha Polisi cha Mbozi, alimuomba mbunge wa eneo
husika avute subira ili waweze kuona namna bora ya kufanya kwani bajeti ya
Serikali ni ndogo na vituo vinavyotakiwa kujengwa ni vingi.i
No comments