Madiwani wa Misungwi Watoa Tamko Zito Kuhusu Kutumbuliwa kwa Mbunge Wao Charles Kitwanga...........Wanataka Bunge Limuombe Radhi



UTANGULIZI
Ndugu Waandishi wa habari, Karibuni kwenye mkutano huu mfupi ambao lengo
lake ni kutoa taarifa yetu fupi kuhusu ukweli uliojificha kuhusu kitendo
kilichopelekea Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri
wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Tunaamini kwa uwezo mliona kama waandishi wa habari, taarifa hii itafikia
umma wa Watanzania kama ilivyokusudiwa.
UFAFANUZI
Kama mnakumbuka mnamo tarehe 20 Mei mwaka huu, Rais Dk John Pombe
Magufuli alichukuwa uamuzi wa kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya
Ndani, Charles Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Misungwi kwa kosa la
kwamba Mhe. Kitwanga aliingia bungeni akiwa amelewa.
Sisi wananchi wa Jimbo la Misungwi tumesikitishwa sana na taarifa na uamuzi
huu kwa kuwa tunaamini kuwa kuna dhamira iliyojifika iliyopelekea Mhe Rais
kufanya maamuzi haya.

Ukweli ni kwamba huu ulikuwa mpango wenye dhamira ovu na uliogubikwa na
uongo mwingi ukilenga kumchonganisha Mbunge wetu na Mhe. Raisi
uliopangwa na waovu wachache ambao wamebanwa na Serikali hii ya Awamu
ya tano kupitia wizara hiyo nyeti kwa usalama wa nchi.
Itakumbukwa kuwa, Mhe Charles kitwanga alinadiwa na Mhe Rais na wanaCCM
na baadae kupigiwa kura kwa wingi na wananchi wa Misungwi kwa ajili ya
uwezo wake na dhamira yake njema ya kulinda taifa letu.
Sisi wananchi wake, tunaamini katika uwexo wake, uadilifu wake na nidhamu ya
kazi aliyonayo, hatuna mashaka na hili.

Baada ya kuteuliwa na Mhe Raisi kama Waziri wa mambo ya ndani, amekuwa
muadilifu na kafanya mengi katika kuimarisha usalama na kufanya maamuzi
yengi mazuri kwa maslahi ya taifa.
Hili lilimtengenezea maadui wengi ndani ya serikali, ndani na nje ya CCM,
mtandao wa dawa za kulevya, walioachishwa kazi NIDA na Uhamiaji.
Watu hawa ndio waliochochea na kutengeneza mkakati wa kumchafua Mhe
Kitwanga na walikuja dodoma kuhakikisha dhamira yao ovu inatimia.

USHAHIDI WETU
Miongoni mwetu tulikuwa mjini Dodoma pamoja na madiwani wa Jimbo la
Misungwi ambao tulikwenda kumtembelea Mbunge wetu bungeni, tulizungumza
mengi kwa ajili ya jimbo letu na katika kikao chetu hapakuwa na chembe ya
kilevi chochote na hata kesho yake alipoinga bungeni alikuwa mzima wa afya
ya kimwili na akili timamu na tunawahakikishieni kuwa Kitwanga hakuwa
amelewa.
Ndugu waandishi wa habari asubuhi ya tarehe 20 tulielekea bungeni kwa
mwaliko wa Charles Kitwanga, tukiwa sehemu ya mualiko uliowajumuisha
Madiwani wa jimbo lake tukiwa tumeambatana naye tukaingia ndani ya ukumbi
wa bunge,tukashuhudia anajibu swali,baada ya kujibu swali la mbunge
Sakaya,tulitoka nje na kupiga picha na madiwani wote wa Misungwi waliokuja
kumtembelea Dodoma.

Baada ya zoezi la kupiga picha kukamilika pale nje ya ukumbi wa Bunge,
tulitoka na kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kututembeza
maeneo yote ya Dodoma , lakini ilipofika jioni wakati tukirejea nyumbani tukiwa
naye, ghafla tukaona habari zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa
Waziri Kitwanga amevuliwa uongozi kwa kuwa alionekana na Waziri Mkuu
akiwa amelewa.
Ndugu wanahabari , tulishangazwa wote kwani tulikuwa tumekaa naye pale
nyumbani kwake Dodoma (site 2) tukipata chakula cha usiku ,alionekana
kutoaamini na hata madiwani pia na wengine ambao tulikuwepo hapa nyumbani
kwake hatukuamini.

Tunachosema ni kwamba waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo
imepotoshwa, bali ulikuwa ni mkakati wa kumchafua na kuhakikisha anavuliwa
wadhifa wake ili watu hawa waendelee kufanya maovu yao.
Mtandao wa dawa za kulevya, pamoja na wale waliokuwa wanamshutumu
kwamba amehusika kuondolewa kwao kazini wakiwemo Watu wa NIDA, Mbunge
wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Mfanyabiashara Said Lugumi pamoja
na kundi mafisadi waliokwapua mabilioni ya fedha NSSF.
Pia na baadhi ya wabunge wa CCM na Upinzani ambao walikuwa
hawafurahishwi na kasi ya utendaji kazi wa Kitwanga katika Wizara ya Mambo
ya ndani.

Kwa niaba ya wananchi wenzetu tunamuomba na kumtahadharisha Mhe. Rais
awe makini na makundi la wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, pamoja na
lile kundi la wanamtandao masalia ndani ya CCM na serikalini na kwenye
vyombo nyeti vya ulinzi na usalama, ambayo kwa ujumla yalikuwa na mkakati
kabambe wa kuhakikisha wanamtenganisha na kumpotosha Mhe Raisin a
kumjaza habari zisizo za kweli.

Ndugu waandishi wa habari, kilichotushangaza zaidi baada tu ya Kitwanga
kuvuliwa madaraka yake ya uwaziri, kuna watu walianza kufanya sherehe
wakishangilia hususani wale waliovuliwa madaraka NIDA pamoja na
NSSF,Uhamiaji na wale wanaotuhumiwa kuhusika na madawa ya kulevya.
Ndugu waandishi wa habari, tunajua namna kundi la Said Lugumi, Ridhiwani
Kikwete na kampuni yao walivyokuwa wanadhamini kwa mbinu za kifedha
katika vita hii ya kitwanga ili aondolewe, lakini baada ya kuondolewa,
wakajifanya kutoa taarifa ya kushangazwa kuondolewa kwake,
Kitwanga amekuwa mtumishi wa serikali akiwa mtumishi mwandamizi benki
kuu Tanzania (BOT),amekuwa mbunge na Naibu waziri kwa miaka 10,lakini
hata siku moja hakuwahi kuonekana amelewa. Ni muadilifu na ana nidhamu ya
kazi, na nidhamu hii ndiyo iliyomfanya aaminiwe na kupewa dhamana hii.

MAAZIMIO YETU
=Tunaliomba Bunge kumuomba radhi Mhe. Charles Kitwanga kwa
kumdharirisha mbele ya wapiga kura wake wa Jimbo la Misungwi familia yake
pamoja na watanzania wote waliokuwa wanaamini utendaji wake kupitia video
iliyochezewa na wataalamu wa IT katika studio za Bunge ili kufanikisha lengo la
kumuonyesha Kitwanga kuwa alikuwa amelewa bungeni.
=Tunamuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa
Serikali bungeni atoe uthibitisho wa kikemia unaotanabaisha wazi kama
Kitwanga alikuwa katumia kilevi wakati akiwa bungeni maana hakuna kipimo
chochote kilichofanyika kudhibitisha uvumi huu.

=Tunaliomba Bunge lifanye uchunguzi na kubaini wale wote waliosambaza ile
video inayoonyesha Kitwanga akiwa anaongea na kuonekana amelewa wakati
kiuhalisia hakulewa na alijibu maswali yote vizuri
=Tunaliomba Bunge kuchunguza idara ya habari ya Bunge pamoja na studio ile
ya Bunge ambao wamehusika na kuhariri ile picha ya video iliyokuwa
inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
=Tunahoji uhalali wa kumvua mtu madaraka kwa sababu ya ulevi bila
uthibitisho wa daktari ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka hayo kugundua
kilevi cha mtu.

= Tunaomba Watanzania wote waliosikitishwa na taarifa hizi wajue tu kwamba
ile video ambayo imemtia hatiani Kitwanga ilihaririwa kwa ustadi mkubwa
kupitia wafanyakazi wa Bunge ambao wanapitia zile asadi za bunge pamoja na
baadhi ya wafanyakazi wa serikali kwenye vyombo vya ulinzi na usalama
ambao hawakupenda kitwanga aendelee kuwa pale ,kwa nia ya kumhujumu na
sasa wanasema kwenye vyombo vya habari ili kuhalalisha uhujumu huo.
=Tunaomba mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kuangalia picha
zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Mhe Mbunge wa
Misungwi ambazo zinaonekana kumchafua wachukue hatua dhidi ya watu hao
kwani kisiasa zinaendelea kumchafua na kumharibia kwa wapigakura
wake,familia yake,mama yake mzazi ,ndugu zake .

=Tunajiandaa kuchukua hatua kwa Bunge za kisheria kama watashindwa
kuthibitisha tuhuma hizo dhidi ya Charles Kitwanga ambazo tunaamini
zimetengenezwa kwa maslahi ya makundi yanayompinga ndani ya Serikali
wakiwemo mtandao wa dawa za kulevya.

Pia tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa makini
kundi la wanamtandao walio ndani ya serikali ambalo linaongozwa wahafidhina
wasio taka mabadiliko ndani ya serikali .
Imeandaliwa na madiwani wa Jimbo la Misungwi pamoja na wakereketwa wa
jimbo hilo.Baraka Kingamkono,Gaudency Tungaraza na IDDY Majumuisho.
Asanteni na Mungu awabariki.

No comments