Rais Magufuli Azungumzia Sakata la Wanafunzi Waliotimuliwa UDOM.......Ashangaa Fedha za Mikopo kupelekwa kwa ‘Vilaza’



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amesema
kuwa baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walioondolewa chuoni
hivi karibuni hawakuwa na sifa za kujiunga na masomo chuoni hapo.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya Kisasa katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli amewataka watanzania kuweka siasa
kando nakuzungumzia masuala ya msingi, huku akiwashangaa wanasiasa
waliojitokeza kuwatetea wanafunzi hao.

“Nimeshukuru wale vijana wameondoka. Wanasiasa haohao, ‘eti ooh.. hao
vijana wamekosa pa kulala.. it’s nonsense’. Taifa letu tuliweke mbele kwanza.
Siasa zije nyuma,” alisema.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi ambao walibainika kuwa na elimu ya kidato
cha nne waliofeli masomo yao na kuruhusiwa kuendelea na masomo ya elimu
ya juu ni watoto wa viongozi.

“Ukimchukua mtoto wa form four ukampeleka pale, hata kama atafanikiwa
kupata degree… itakuwa ya ajabu. Na baadhi ya watoto waliopelekwa pale ni
watoto wa viongozi. Watoto wa Maskini wenye qualification wamekosa nafasi
za kwenda Chuo Kikuu. Watoto wa watu fulani fulani wanapelekwa wakati
walifeli. It can’t be,” Dk. Magufuli alisisitiza.

Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali yake haitaruhusu fedha zinazopaswa
kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kupelekwa kwa ‘vilaza’ huku
waliofaulu wakikosa mikopo ya elimu ya juu.

Dk. Magufuli ameahidi kuwa Serikali yake itahakikisha wanafunzi waliofaulu kwa
kiwango cha daraja la kwanza na la pili (division 1 &2) wanajengewa mazingira
mazuri ya kuendelea na masomo.
“Waliofeli watafute vyuo vyenye size yao,” alisisitiza



No comments