Janga la Watumishi hewa Mwanza
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema watumishi hewa 367 kati
ya 1057 wamebainika kutafuna zaidi ya Sh. bilioni 2 mkoani humo.
Ulipaji wa mishahara watumishi hewa unadaiwa kufanywa na baadhi ya wakuu
wa idara na wakuu wa vitengo wasiokuwa waaminifu huku wengine
wakituhumiwa kupokea fedha zilizokuwa zikitolewa.
Mkuu wa mkoa John Mongella ameyasema hayo mbele ya Susan Mlawi, Naibu
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma wakati wa
maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.
Mongella amesema, kumekuwepo na baadhi ya wakuu wa idara na wakuu wa
vitengo mkoani humo wasiokuwa waaminifu ambao wamesababisha kuendelea
kuwepo kwa watumishi hewa, kitendo ambacho alidai hakitafumbiwa macho.
Amesema kuwa, katika uhakiki wa watumishi hewa katika mkoa huo, ulioanza
Aprili 18 na kumalizika Juni 3 mwaka huu, umefanikiwa kuwapata watumishi
hao hewa huku wengine wakiendelea kulipwa mishahara.
“Kuna watumishi wa 13 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri
ya Kwimba ambao wamekopa mikopo benki na wakati hawapo katika utumishi
wa umma na wanaofanya hayo ni wakuu wa idara.
“Pia kuna watumishi 72 ambao wamelipwa mapunjo ya mishahara katika
halmashari ya Wilaya ya Magu kupitia akaunti zao za benki na vilevile
wakalipwa tena kupitia dirishani (Double payment) na kila mmoja alikuwa
analipwa zaidi ya milioni tatu,” amesema Mongela.
Mongela amesema, kutona na kuwepo kwa watumishi hao, ofisi yake inakusudia
kuwafuta watumishi wote wasiojulikana kwa waajiri, kuwafuta kwenye malipo
watumishi waliofariki, walioacha kazi waliofukuzwa kazi na waliostaafu.
Wengine watakaofutwa ni waliogombea nafasi tofauti ikiwemo ubunge,
kuwachukulia hatua maofisa wa halmashauri waliohusika kuanzisha na
kuidhinisha mikopo kwa watumishi waliotoka katika utumishi wa umma.
Hatua nyingine zitakazochukuliwa ni kuhakikisha watumishi waliolipwa mapunjo
ya fedha za mishahara zaidi ya stahili zao zinarejeshwa, kuwachunguza na
kubaini maafisa na wasimamizi wa watumishi waliosababisha upotevu wa
fedha kupitia malipo ya mshahara wa watumishi hewa.
Hata hivyo Mongella amesema, Februari mwaka huu watumishi hewa waliolipwa
mshahara katika sekretarieti ya mkoa na halmashauri walikuwa 28,068,
halmashauri 27, 416 na katika sekretarieti ya mkoa walikuwa 652 huku
watumishi wa halmashauri waliohakikiwa ni 26, 359 ambao hawakufika
kuhakikiwa ni 1,057.
Na kwamba licha ya kutolewa kwa tangazo la kuwaita watumishi wote, waliopo
masomoni, likizo na waliohama vituo vyao vya kazi lakini wengine hawakuweza
kutekeleza agizo hilo jambo ambalo linaonesha wazi ni watumishi hewa.

No comments