Jeshi la Polisi laua vinara wa mauaji Tanga, Mwanza
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo limeeleza kumuua Salum
Saidi Muhangwa (30) kwa madai ya kuwa miongoni mwa waliofanya mauaji
kwenye msikiti huo.
Akizungumza na wanahabari Simon Siro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam amesema, mtu huyo ameuawa leo asubuhi wakati akijaribu
kuwakimbia polisi kupitia dirishani.
“Baada ya kufanya mauaji kule Mwanza na kikundi chake walikimbilia huku Dar
es Salaam, taarifa za raia wema zimetuonesha jambazi huyo alikua anaishi
Buguruni,” amesema.
Mauaji hayo yalifanyika tarehe 19 Mei mwaka huu katika msikiti huo uliopo
kwenye Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana ambapo watu watatu, waumini
wa msikiti huo waliuawa wakati mwingine mmoja akijeruhiwa.
Kamanda Sirro amesema, mtu huo baada ya kugundua kuwa askari
wamezunguka jengo alilikuwemo, alijaribu kujihami kwa kuwarushia askari bomu
la mkono ambapo askari walifanikiwa kumpiga risasi ya mguu hatimaye kufariki
wakati akipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
“Tunashukuru askari hawakufanywa lolote katika tukio hilo na tunashukuru kwa
sababu wapo makini,”amesema Kamanda Sirro.
Hata hivyo amesema, mtu huyo amefanya matukio mengi pale Mwanza
yakiwemo kufanya unyang’anyi katika vituo vya M-Pesa, Tigo Pesa, uchinjaji
watu msikitini pamoja na maduka makubwa.
“Kuna timu yake imebaki hapa Dar es Salaam lakini tuwahakikishie wana Dar es
Salaam kwamba, tutawakamata na haki itatendeka lakini wakikaa vibaya
wasilaumu serikali.
“Kwa sababu silaha wanazozitumia hawajanunua madukani, wanakaa nazo
visivyokua halali wabadilike wawe raia wema itawasaidia lakini kwa staili hii
niwaambie wataacha familia zao kwa sababu ukamataji wa mtu mwenye silaha
sisi ndio tunajua namna ya kukamata,”amesema.
Katika tukio jingine, Jeshi hilo limefanikiwa kumuua jambazi sugu aliyefahamika
kwa jina la Mohamed Abdallah akiwa na bastora aina ya nolinko, risasi 19 na
bomu la kutupa kwa mkono.
“Baada ya kufanya mauaji Tanga na kikundi chake walikimbilia hapa Dar es
Salaam, naye akachomoka na kuanza kupambana na polisi, na askari wetu
waliweza kumjeruhi vibaya sana naye wakati akipelekwa hospitali alifariki
dunia.
Kamanda Siro amesema mtu huyo ni kiongozi mkubwa aliyebaki katika kundi la
majambazi mkoani Tanga na amehusika katika mauaji ya watu wanane pamoja
na ujambazi uliofanyika katika kituo cha mafuta mjini humo.
“Wananchi na hasa raia wema waendelee kutupa taarifa kwa watu
wanaowatilia mashaka,” amesema

No comments