Yanga yachapwa nyumbani 28-06-2016

Ikicheza kwenye dimba lake la nyumbani mbele ya mashabiki zaidi ya elfu
arobaini waliofurika kwenye dimba la Taifa, wawakilishi wa Tanzania katika
michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika Yanga wamechapwa bao 1-0 na
TP Mazembe.

Yanga imepoteza mchezo wake wa pili mfululizo katika kundi A linaloongozwa
na TP Mazembe iliyofikisha pointi sita.
Yanga ilichapwa bao 1-0 na Mo Bejaia ya Algeria katika mchezo wake wa
kwanza uliopigwa nchini Algeria.

Licha ya kupoteza mchezo wa leo, Yanga imezidi kuimarika kwani iliweza
kuwadhibiti vijana Moise Katumbi kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili TP Mazembe ilirejea kwa nguvu, huku Thomas Ulimwengu
akiisumbua sana ngome ya Yanga.

Uzoefu wa mabingwa hao mara tano wa Afrika ndio uliofanya klabu hiyo itoke
na ushindi kwenye dimba la Taifa.

Licha ya uwanja kuonekana kufurika mashabiki wa Yanga waliokuwa wamevalia
mavazi ya timu hiyo, kulikuwa na idadi kubwa ya washabiki wanaodhaniwa
kuwa wa Simba ambao walikuwa wakishangilia klabu ya TP Mazembe tangu
mwanzo wa mpambano huo.

Yanga itacheza mchezo wake dhidi ya Medeama ya Ghana July 15, italazimika
kushinda mchezo huo kuweka hai matumaini yake madogo ya kutinga nusu
fainali.




Y

No comments