MSAKO MKALI WAENDESHWA MKOA PWANI.

MTAA wa Mwendapole B wilayani Kibaha mkoani Pwani umeendesha msako wa kuwakamata vijana watatu waliounda kikundi cha uhalifu kijulikanacho kama askari wa kirusi au Bora ufe kuliko unyonge.

Kundi hilo lilivamia shule ya sekondari ya Simbani Juni 2  mwaka huu huku wakiwa na mapanga na marungu na kuwatishia wanafunzi wa shule hiyo wakidai kuwa wanamnyanyasa mwenzao hata hivyo walitokomea vichakani baada ya kubaini polisi wamefika shuleni hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa mtaa huo Guudluck Manyama alisema kuwa vijana hao walikamatwa kwenye msako uliofanyika kwenye mtaa huo.

Manyama alisema kuwa vijana waliokamtwa ni watatu kati ya 11 wanaounda kundi hilo ambao wanakaa kwenye mtaa huo na kundi hilo linaundwa na vijana wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 na wengi wao ni wale ambao waliacha shule.

Aliwataja vijana hao kuwa ni Said Ndunguru, Said wa Mbinguni na Shaib Kilowile huku wengine wakiendelea kutafutwa ambao ni Jamaly Bacha, na Mathias ambaye anatokea mkoani Arusha na inasadikiwa kuwa ni kiongozi wa kundi hilo, Ramdhan Bura, Seleman Beberu, Abdala Lusekelo, Mohamed Beberu na Nasib Mansuri.

“Tunakumbana na changamoto kubwa ya kuwakamata vijana hawa kutokana na baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wao au kuwatorosha lakini hata hivyo tunaendelea kuwatafuta na watakapopatikana watapelekwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema Manyama.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa wanendelea kufuatilia vijana hao ili kuwakamata na mkondo wa sheria uweze kuchukua nafasi yake.

Mushongi alisema kuwa tayari amepata taarifa hizo na kuwataka vijana hao waachane na uhalifu bali wafanye shughuli halali za kuwapatia kipato lakini siyo uhalifu na watashirikiana na polisi jamii kwenye mataa huo ili kuwatokomeza kabisa vijana hao.
































No comments