VIJANA WA JAMII YA WAFUGAJI WACHANGIA DAMU PWANI.

Vijana wa Jamii ya Kifugaji Vigwaza Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani .

BAADHI ya vijana wa kabila la wafugaji wa Kimasai kutoka Vigwaza wilayani Bagamoyo wamejitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia watu ambao wanakabiliwa na upungufu wa damu kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha.

Kabila hilo la Kimasai limekuwa na utamaduni wa kuogopa kutoa damu kutokana na dhana iliyojengeka kwa jamii hiyo kuwa endapo watatoa damu watapoteza maisha jambo ambalo limewafanya Wamasai kutokuwa na utamaduni wa kujitolea damu kwa ajili ya wagonjwa.

Akizungumza mara baada ya kumaliza zoezi hilo moja ya vijana waliojitokeza Pororeti Damson alisema kuwa watu wa kabila lao ni waoga kutoa damu kutokana na dhana kuwa endapo watatoa damu watakufa hali ambayo imejenga hofu ya kujitolea damu kwa ajili ya wagonjwa hata wale wanaotoka ndani ya familia zao.

“Endapo mwanafamilia anakuwa amepungukiwa na damu huwa tunanunua watu kwa ajili ya kututolea damu lakini sisi wenyewe siyo rahisi kujitolea damu kutokana na dhana hiyo ambayo imejengea hofu ya kufanya zoezi hili ambalo tumelifanya na kuwa mfano kwa wenzetu,” alisema Damson.

Naye Meshack Sungaloi alisema kuwa wakati akisubiri kujitolea damu aliingiwa na hofu kubwa akiogopa kuwa huenda yanayosemwa yakatokea lakini alipoanza zoezi hilo hofu iliondoka na kuona kuwa ni jambo la kawaida na si kama wanavyosema watu wengine ambao wamekuwa wakiwatisha kuwa watapoteza maisha endapo watafanya hivyo.

Kwa upande wake Feliciana Mmasi ambaye anatoka kitengo cha lishe kwenye hospitali hiyo alisema kuwa jamii ya Kimasai imekuwa ikiathirika na upungufu wa damu hasa kwa watoto na mama wajawazito kutokana na kutokula vyakula vinavyoongeza damu ambapo wamekuwa wakinywa damu ya ngombe au mbuzi kwa madai ya kuongeza damu jambo ambalo halina ukweli.

Mmasi alisema kuwa ili mtu aongeze wingi wa damu napaswa kula vyakula vya aina zote ikiwa ni pamoja na nyama, mboga za majani, samaki na dagaa lakini wao wamekuwa wakila chakula cha aina moja ambayo ni nyama pekee hivyo watoto wengi kukabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa damu.

Naye Elicia Towo ofisa muuguzi wa Hospitali hiyo kitengo cha damu salama alisema kuwa uelewa kwa jamii hiyo ya wafugaji wa kabila la Kimasai bado ni mdogo jambo ambalo linawafanya kuwa na imani hiyo ambayo imepitwa na wakati.

Towo alisema kuwa wanapinga na utaratibu wa baadhi ya watu wa jamii hiyo kuwa na utamaduni wa kununua damu badala ya kujitolea kwani damu ya knunua kwa watu siyo nzuri bali ni vema wakawa na utamaduni wa kujitolea damu na kuachana na dhana potofu ambayo imjengeka kwa jamii hiyo.

Awali akielezea juu ya kujitolea damu Mchungaji wa kanisa la Gosheni ambao ndiyo waliowahamasisha vijana hao kujitolea damu, Jackson Bukelebe alisema kuwa amefikia hatua ya kuhamasisha watu wa jamii hiyo kujitolea damu ili kuwasaidia wagonjwa.

Mch Bukelebe alisema kuwa kujitolea kwa vijana hao ni mfano mzuri na wao watakuwa mabalozi kwa jamii hiyo ili iwe na utamaduni wakujitolea damu hasa pale ndugu zao wanapohitaji damu kuliko kuwa na utamaduni wa kuona kuwa damu ina nunuliwa.

No comments