Lissu afikishwa Mahakamani







Mwanasheria wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Tundu Lissu
ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ameseme kuwa,
vitendo vinavyofanywa na serikali ya awamu ya tano ni vya hovyo.

Lissu ameyasema hayo muda mfupi baada ya kumaliza kusikiliza shauri lake
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam
Kwenye shitaka hilo, Lissu pamoja na washitakiwa wengine watatu wanadaiwa
kufanya makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchochezi kupitia gazeti la
Mawio la tarehe 14 Januari 2016.

Kwenye gazeti hilo lililoandikwa kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’
Lissu alinukuliwa kama mchangiaji wa gazeti hilo ambapo tayari limefutwa na
serikali.

Nje ya mahakamani hiyo Lissu amesema “nchi yetu imeingia katika giza nene,
mambo yanayofanywa na Serikali hayakubaliki.

“Kila msema kweli wa nchi hii, huu ni wakati wa kujitokeza na kusema hii ni
nchi ya vyama vingi, hii ni nchi inayotambua haki za binadamu kwenye Katiba
yake.

“Hatuwezi tukakubali nchi iongozwe kwa kauli za mdomo za mtu mmoja hata
kama amechaguliwa kuwa rais.”
Akizungumzia kesi iliyofunguliwa na kuhusishwa kwake Lissu amesema, kesi
iliyofunguliwa na serikali dhidi yake na wahariri wa gazeti la Mawio ya
uchochezi, ni ushahidi tosha kuwa nchi imeingia kwenye giza nene la
udekikteta.

Amesema, hata sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ipo wazi kwamba, kuikosoa
serikali sio uchochezi.

“Mashtaka haya yanayodaiwa kuwa ni ya uchochezo, sio ya uchochezi hata
kidogo. Nilichosema, niliulizwa na waandishi … nilisema uchaguzi wa marudio
Zanzibar unaweza kuviingiza visiwani hivyo kwenye machafuko na umwagaji
damu… ni kauli ya raia anayefahamu na hapendezwi na mwenendo wa serikali”
amesema Lissu.

Amesema kuwa, hata sheria ya magazeti inasema kuwa kitendo chochote
chenye lengo la kueleza ubovu wa serikali au mamlaka yake sio kosa.
“Nilichosema mimi kuwa serikali hii na matendo yake ni ya hovyo… hali hii
inahitaji kupingwa na kila mwananchi,” amesema.

“Kama wanafikiria watatutisha kwa kutuleta mahakamani, tutamkabili
mahakamani na tutamkabili nje.
“Ni wakati wa wazalendo kusema kuwa, Tanzania ni nchi ya vyama vingi na ina
Katiba na sheria.

"Katiba yetu inatambua haki za binaadamu na moja haki za binaadamu ni
kueleza ujinga wa watawala wanapofanya ujinga,” amesema.






No comments