Waziri Mkuu Awataka Viongozi Wa Dini Kushirikiana Na Serikali Kupambana Na Rushwa, Ufisadi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini
kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazoikabili zikiwemo za rushwa, ufisadi na
matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema siku zote kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya
Serikali na Asasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na madhehebu ya
Dini katika kuwapatia huduma za kijamii kama vile, afya, elimu,
maji, utunzaji wa mazingira na nyingi nyingine.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana mchana (Jumapili,
Juni 12, 2016) wakati alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dk.
John Magufuli katika Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa
kuwa Mhashamu Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa
Jimbo Katoliki Geita.
“Serikali inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Kanisa
Katoliki katika Jimbo hili la Geita na Tanzania kwa ujumla hivyo
wito wangu kwa Baba Askofu na Waumini wa Kanisa kwa ujumla
wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya kutoa
huduma muhimu kwa jamii,”alisema.
Alisema maendeleo ya nchi yanawategemea wote hivyo
ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali utawezesha maendeleo ya
Taifa kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha wananchi wote.
Waziri Mkuu alisema jukumu la Serikali ni kuweka mazingira
wezeshi ambayo yatasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini
na kwamba kazi kubwa ya viongozi wa dini kuunganisha jamii
na wala siyo kuwatenganisha.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema kinachotakiwa kufanywa na
wote ni kumwuomba Mwenyezi Mungu awawezesha kuwaelewa
viongozi walioko madarakani na kutii maelekezo yanayotolewa
kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii mamlaka.
Alisema iwapo waumini watatii na kuzingatia mafundisho ya
kiroho yanayotolewa na viongozi wao wa dini ni dhahiri
kwamba yatajenga imani miongoni mwao na upendo utatawala
katika jamii nzima.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kushirikiana na
Madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania wote bila
ubaguzi, hivyo aliwasihi waendelee kuwekeza katika huduma za
jamii ikiwemo Shule, Vyuo, Zahanati kwa kuwa wana jukumu la
kushirikiana kwa pamoja kujenga taifa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu aliwaomba wote kwa pamoja
waunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika
kupambana na uzembe, ubadhirifu na wote wanao kiuka maadili
ya utendaji wa kazi.
Kwa upande wake Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo la Bunda
ambaye alikuwa msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Geita
amewaomba waumini kumpa ushirikiano Askofu mpya wa jimbo
hilo.
IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JUNI 12, 2016.xaitogifucvk
No comments