CHAWAMAPIKI WAFANIKIWA KUKABILIANA NA UHALIFU.
CHAMA Cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki (CHAWAMAPIKI) kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani kimefanikiwa kukabiliana na uhalifu kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoa wa Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti Hussein Kijazi alisema kuwa ushirikiano huo umetokana na kuanzisha utaratibu wa kila mwendesha bodaboda anakuwa na koti maalumu la kumtambulisha ambalo linakuwa na namba mgongoni hivyo kupunguza matukio ya wizi ambayo yalikuwa yakiwahsirikisha waendesha pikipiki.
Kijazi alisema kuwa zoezi la kuwapatia makoti madereva hao umesaidia kwani baadhi ya madereva boda boda walikuwa wakitumika na wezi kufanya uhalifu au wenyewe kushiriki kwa kuwapora abiria wao.
“Tunalishukuru jeshi la polisi kwa kutuunga mkono na kufanikisha kupunguza matukio ya uhalifu ambapo madereva wa bodaboda walikuwa wakihusishwa kushiriki uhalifu wakishirikiana na watu ambao si wema, polisi wamekuwa wakitupa ushirikiano wa hali ya juu,” alisema Kijazi.
Alisema kuwa kwa sasa waendesha bodaboda wamebadilika kupitia chama hicho na kadiri muda unavyokwenda wanakuwa vijana wazuri kutokana na chama kudhibiti wale ambao ni wakorofi.
“Kwa sasa tuna malengo ya kuanzisha sehemu ya kuoshea magari ili iwe mradi wa kukiongezea chama mapato yake ambapo kwa sasa mradi uliokuwepo ni wa makoti ambao si wa kudumu hivyo tukifanikiwa kuanzisha mradi huu utatusaidia kuongeza mapato,” alisema Kijazi.
Aidha alisema kuwa mbali ya kujenga nidhamu ya wanachama ili kuhakikisha wanafuata sheria za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuwatafutia mafunzo ya udereva ili wapate leseni wawe kisheria zaidi kuliko kuendesha kiholela.
Amebainisha kuwa chama hicho kinawasaidia wanachama hasa katika matatizo ikiwa ni pamoja na ajali mwanachama hulipwa kiasi cha shilingi 50,000 kwa ajili ya matibabu na anapokufa hufanikisha mazishi yote ikiwa ni pamoja na 100,000 ambapo kina wanachama 500 huku wenye leseni wakiwa 400.
No comments