WATU 21 WAFA KWA UGONJWA WA AJABU NGORONGORO
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Ghambo |
| Na Vero Ignatus Arusha
Wakati watu
zaidi ya 21 wamekufa katika kata ya Pinyinyi wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha
kwa ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Frida Mtiki
hana taarifa juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo.
Hayo
yalisemwa na Mtendaji wa kata hiyo,James Mushi wakati akisoma risala kwa Mkuu
wa Mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo alipokwenda kutembelea kata hiyo kujionea
shughuli za maendeleo ikiwa ni ziara ya siku tano katika wilaya hiyo.
Baada ya
Mushi kueleza katika risala yake juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo kwa zaidi ya
miaka minne na watu 21 kupoteza maisha ndipo Mkuu wa Mkoa alipomsimamisha
Mganga Mkuu wa Mkoa ili kupata maelezo ya kwa nini Mkoa haujachukuwa hatua.
Mganga huyo
alisimama na kuueleza umma wa wananchi waliohudhuria Mkutano huo wa hadhara
kuwa hana taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo na wala Mkoa haina taarifa juu ya
kuwepo kwa ugonjwa huo.
Majibu hayo
yalimchanganya na kumkasirisha Mkuu wa Mkoa na kuamua kumsimamisha Mganga wa
Wilaya ya Ngorongoro(DMO),Omari Sukari kutoa majibu kama na na yeye hana
taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo.
Sukari
alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na alikiri kweli umeua watu 21 na amefanya
jitihada na ziada kwa kupeleka sambo Wizara ya Afya kwa wataalamu kwani hata
yeye ameshindwa kujua nini chanzo cha ugonjwa huo na kina sababishwa na kitu
gani.
Mganga huyo
wa wilaya alisema vipimo vya awali vilionyesha kuwa ugonjwa huo husababishwa na
ugonjwa wa kichocho lakini bado wamejiuliza zaidi kwa kupeleka samba nyingine
ya matapishi kwa wataalamu wa magonjwa ya binadamu kujua zaidi ukweli wa
ugonjwa huo na majibu hayajarudi.
Baada ya
majibu hayo,Mkuu wa Mkoa alieleza waziwazi kusikitishwa na kushangazwa majibu
ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kusema kuwa haingii akilini ugonjwa ulioua
watu 21 na uko zaidi ya miaka minne katika kata ya Pinyinyi lakini hana taarifa
wakati Mganga wa Wilaya anayo taarifa.
Gambo
alisema kuwa hiyo inaonyesha wazi kuwa baadhi ya watumishi wa serikali Mkoani
Arusha wanafanya kazi kwa mazoea na kushindwa kujua ama kupata taarifa za kila
siku katika wilaya.
Alisema hilo
hatalivumilia hata kidogo na kuwataka wakuu wa idara wa mikoani kuwajibika kwa
kupata taarifa za kila siku katika wilaya zote za mkoa wa Arusha ili majibu ya
kila kitu yaweze kupatikana na kupatiwa ufumbuzi wa kutosha.
’’Hii ni
aibu ugonjwa upo kwa miaka minne na tayari umeua watu 21 lakini RMO hana
taarifa lakini DMO anayo taarifa na amefanya kazi ya ziada kutafuta chanzo cha
ugonjwa huu’’ alisema
’’Kama
nisingekuja hapa ina maana huu ugonjwa usingejulikana wala kupata majibu ya
kutosha na watu wangeendelea kufa sasa nataka RMO kuhakikisha ugonjwa huo
unakwisha na dawa inapatikana’’ alisema Gambo
Katika
risala hiyo wananchi wamempongeza mkuu huyo wa Mkoa wa kufika katika kata hiyo
kwani mara ya mwisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha kutembelea kata hiyo alikuwa Mkuu
wa Mkoa, Mohamed Babu mwaka 2006
|

No comments