Mkuu wa wilaya ya Kibaha aweka kipindi cha mpito kwa wafugaji
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumpter
Mshama ameweka kipindi cha mpito kwa wafugaji wa wilaya hiyo kutoingiza mifugo
kwenye mashamba ya wakulima wakati serikali ikiangalia namna ya kumaliza
migogoro baina yao na wakulima.
Amesema hayo ofisini kwake mjini Kibaha wakati
alipokutana na viongozi wa wafugaji baada ya agizo lake la kuwataka wafugaji
kupunguza mifugo yao pia kwenda kwenye maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili yao
ambapo alitoa mwezi mmoja toka Septemba 15 hadi Oktoba 15 mwaka huu kwa
wafugaji kwenda kwenye maeneo yao kupunguza
migogoro baina yao na wakulima.
Alisema kuwa katika kipindi hicho cha mpito kabla
ya maamuzi mengine hayajachukuliwa hawapaswi kulisha mifugo kwenye mashamba ya
wakulima na endapo watafanya hivyo ngombe watakaoingia kwenye mashamba
watagawana na wakulima walioharibiwa mazao yao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud
Jumaa alitaka maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji yaainishwe ili kupunguza
migogoro hiyo ambayo kwa sasa imekithiri wilayani humo.
Jumaa alisema kuwa endapo maeneo hayo yataainishwa
itasaidia kupunguza mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha
uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
ya Kibaha Tatu Seleman aliwataka wafugaji kukaa kwenye maeneo yao ambayo
walitengewa.
Seleman amesema kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili
ya wafugaji wenyewe hawayatumii na kutaka kukaa na wakulima jambo ambalo
limeleta sintofahamu kwa pande hizo mbili.
Naye katibu wa chama cha Wafugaji nchini Magembe
Makoye alisema kuwa imefika wakati wafugaji kukubali mabadiliko kwa kufuga
kisasa kwa kutegemea ukubwa wa eneo.
Makoye amesema kuwa kwa sasa mifugo imekuwa ni
mingi huku eneo la kufugia likiwa dogo hali ambayo inasababisha migogoro ya
mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji pia aliomba kuwe na ushirikishwaji
wa maamuzi ya namna ya ufugaji.
Naye mfugaji Amerika Chamiti amesema kuwa ni vema
mipaka iliyowekwa baina ya wakulima na wafugaji ionyeshwe ili kupunguza
migogoro hiyo kwani pande hizo zimekuwa zikiingiliana.
Chamaiti amesema kuwa mipaka ndiyo itakayosaidia
kuanisha eneo la kila upande kwani Halmashauri ilitenga maeneo hayo karibu kila
kijiji lengo likiwa ni kila mtu akae kwake na asiingie kwa mwenzake.
Kikao hicho kimekuja baada ya mkuu wa wilaya hiyo Asumpter
Mshama kutoa mwezi mmoja hadi ifikapo Oktoba 15 wafugaji wote wawe wamekwenda
kwenye maeneo waliyopangiwa pamoja na kupunguza mifugo ili kuepusha migogoro
baina ya wakaulima na wafugaji.
No comments