Wednesday, April 27, 2016 Polisi Temeke Wakamata 'Panya Road 18


Jeshi la Polisi linawashikilia vijana zaidi ya 18 wenye umri kati ya miaka 14 na
20 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Wilaya
ya Temeke.

Kamanda wa polisi wa Temeke, Gilles Muroto amesema leo kuwa vijana hao,
wanaohusishwa na kundi la Panya Road linalofanya unyang'anyi maeneo ya jiji
la Dar es Salaam, walikamatwa jana nyakati tofauti baada ya polisi kuendesha
msako wa kuzuia na kupambana na wahalifu.

Alisema vijana hao wanatoka maeneo ya Buza Kanisani, Chanika, Yombo
Kirakala, Buza Changulu, Yombo Makangawe na moja anayeishi maeneo ya
Mwananyamala lakini alikamatwa Temeke.

"Kama Kamanda Simon Sirro alivyosema kuwa ni lazima wahalifu wadhibitiwe
katika mko huu. Temeke hatuwez kumwangusha, tunatekeleza agizo lake,"
alisema Kamanda Muroto.

Alisema vijana hao wanajihusisha na vitendo vya uporaji wa mali mbalimbali
kuanzia mitaani, pia kujeruhi watu hali inayosababisha wakazi wa eneo husika
kuishi kwa hofu.

Alisema upelelezi ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa
hatua za kisheria.

Wakati huohuo, Kamanda Muroto amesema polisi inashikilia mwanamke mmoja
mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Buza baada ya kumkuta na puli 120 za
dawa za kulevya aina ya bangi.

No comments