Friday, April 29, 2016 Naibu Spika Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumwita Mbunge BWEGE


Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa
kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua
kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said
Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.
Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka
2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.
Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha
wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka
mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye
msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi;
bwege bwege.”
Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz
yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha
kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya
kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na
hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.
Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye
ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga
maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha
shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.
“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,”
alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati
mjadala ukianza kuwa mkali.
Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa
taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na
Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli
hiyo ya naibu spika.
“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna
wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie
bunge hili kupotosha,” alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati.
Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba?
Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?
Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe
umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na
akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.
Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani
wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.
Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali
kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa
mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa
kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu.
Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa viti maalumu
(Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na kumponda
Nape na uamuzi wa Serikali.
Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa.
“Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape
vuvuzela,” alisema.
“Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa
moja?”
Wakizungumzia tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey
Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya
kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata
kanuni na taratibu za kibunge.
“Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama
ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji.
Alisema mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge
hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria.
Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa
na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu
na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si
sawa kabisa.”
Alisema Bunge linapaswa kuongozwa kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo
inawafanya wabunge wa CCM waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani.
“Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo
akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema.
Kwa takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa
vyama vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi ya Rais
na kurejesha uhai kwenye chombo hicho.
Katika hoja zao jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu
ya Tano kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa
kusitisha matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa
mara kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni
za Bunge.
Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa ufafanuzi wao,
walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa Konde (CUF),
Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa maelezo kuwa ndiye
aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo.
Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala bora na
unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala bora.
“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana nzima ya utawala
bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa ufanisi, tija na kwa uwazi,
uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa watu kwa kufuata utawala wa sheria,”
alisema.
Alisema ni ajabu Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni
wakati nchi haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni,
Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa
kwenye Gazeti la Serikali.
“Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa
maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji
Msigwa.
Alisema licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai
kuwa hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba
wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na
kuukosoa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.
“Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija
bungeni mnakaa kimya.Huwa tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja
humu ndani,“ alisema Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi
Kigwangalla kuwa ni mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama
kuomba mwongozo, kupinga kauli ya mbunge huyo.
Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68 (7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka
Mchungaji Msigwa athibitishe kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri
wanaopingana na uongozi wa Serikali.
Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha 63 (1) (2), kinachomtaka
mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo ama apewe muda na
kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na Mchungaji Msigwa
kuwasilisha ushahidi wao.
Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia?
Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge.
Msigwa: Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio
mwongozo ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa.
Ila tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba.
Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni
zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana.
Akiendelea na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi
yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba
hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na
kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
“Bunge ni mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza
kuminya na kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya
fedha za Watanzania,” alisema.
“Serikali inayokandamiza uwazi ni Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu.
Mnasimama na kusema mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha
nini kuwaonyesha Watanzania hiki mnachokifanya?”
Huku akiipongeza Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya
Kikwete, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii
watu kuzungumza na kusema ukweli.
“Nyinyi mmekuja na ‘hapa kazi tu’, lakini hamtaki kukosolewa. Wakati
tunamkosoa Kikwete wabunge wa CCM mlikaa kimya na kutuzomea, leo
mnaufyata na inaonekana hata Dk Magufuli akidondosha kijiko, mtasimama na
kupiga makofi kwa sababu ya uoga wenu,” alisema Mchungaji Msigwa na
kuwataka wabunge kuhoji mambo kwa maslahi ya wananchi.

No comments