Wednesday, April 27, 2016 Mwenyekiti Aweka Majina HEWA Mradi wa Kuokoa kaya Masikini (TASAF


Wananchi wamemkataa mwenyekiti wa kitongoji cha Mwanogi kijiji cha Bulima,
Kata ya Nyashimo wilayani Busega katika Mkoa wa Simiyu, wakimtuhumu
kuweka majina hewa katika mradi wa kuokoa kaya masikini unaosimamiwa na
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Mwenyekiti huyo wa kitongoji, Ester Ng’ombe anatuhumiwa pia kufanya kazi
kwa ubaguzi wa vyama vya siasa.

Akizungumza katika kikao, mwenyekiti wa kamati ya mipango na fedha ya kijiji
cha Bulima, Zablon Ntinika alisema wamefikia uamuzi wa kumsimamisha kazi
mwenyekiti huyo baada ya uchunguzi walioufanya kubaini majina matano
ambayo ni hewa yakipatiwa fedha.

Alisema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa mwenyekiti huyo
katika utendaji wake wa kazi katika kitongoji hicho lakini wamebaini mengi.
Mwenyekiti huyo anayetuhumiwa, alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema kuwa
yeye hayatambui bali ni siasa za chuki dhidi yake.

Ng’ombe alisema chanzo si majina feki bali ni siasa zinazochochewa na
wanasiasa wa kata hiyo ambao wanataka kuichafua sifa yake ili aweze
kuondolewa na wananchi waliomchagua.

No comments